simulizi

April 24, Kumbukumbu Ya Kifo Cha Papa Wemba. Mfahamu Kwa Undani Zaidi.

on

Jina lake halisi ni Jules Shungu Wembadio Pene Kikumba lakini wengi humfahamu kwa jina la uimbaji wake la ‘Papa Wemba’. Alizaliwa katika eneo la Lubefu – Wilaya ya Sankuru nchini Congo Tarehe 14 Mwezi Juni, 1949.

Gwiji huyo wa muziki wa lingala aliyefariki dunia Tarehe 24 April 2016, alikuwa mmoja wa wanamuziki walioanza muziki wakiwa na umri mdogo sana, ambapo Historia yake inaeleza kuwa alikuwa akimfuata mamayake katika maeneo yenye matanga na hivyo akaibukia kuwa mtunzi wa nyimbo za kuomboleza.

Alikuwa ni miongoni mwa wanamuziki wakwanza kujiunga na bendi maarufu ya Soukous Zaiko Langa Langa ilipoundwa tarehe 24 Desemba 1969 mjini Kinshasa. Wakati huo alikuwa akitumia jina la Jules Presley Shungu Wembadio.

Wakati huo akianza Papa Wemba, jukwaaa la muziki nchini humo lilikuwa limetawaliwa na vigogo wa muziki Franco Luambo wa TPOK Jazz, Tabu Ley Rochereau wa Afrisa, na makundi mengine mapya kama vile Les Grands Maquisards, Le Trio Madjesi, Bella-Bella, Thu Zaina na Empire Bakuba.

Umaarufu wa kundi la Zaiko Langa Langa ulipungua miaka ya sabini, na hapo ndipo Shungu alibadili jina lake na kuanza kuitwa jina la utani ”Papa Wemba” badala ya Shungu Wembadio alilokuwa akitumia awali.

Jina hilo la Papa Wemba liliaminika kuwa lingemtambulisha kote duniani, ambapo Nyongeza ya “Papa” kwa maana ya baba kwa lugha ya Kiswahili,iliashiria kwamba alikuwa na majukumu mengi katika familia akiwa ndiye mtoto wa kwanza katika familia yao kwani wazazi wake wote wawili walikuwa wamefariki tangu miaka ya 1960.

Miaka mitano baadaye alihama kutoka kundi hilo na kujiunga na Isifi Lokole hapo alitunga wimbo maarufu wa Amazon, wimbo aliokiri kumtungia mkewake.

Miaka mingine baadae Alijiunga na kundi lingine la “Yoka Lokole”, kabla yake kuunda kundi lake la Viva La Musica mwaka wa 1977.

Vibao maarufu alivyowahi kuimba ni pamoja na Mwasi, Show me the way, Yolele, Mama, Proclamation, Chouchouna, Eluzam na  Mbeya Mbeya (Evoloko Lay Lay), BP ya Munu (Efonge Gina), Mwana Wabi , Mizou (Bimi Ombale) , Zania (Mavuela Somo), Emotion, Wake Up, Maria Valencia, Le Voyageur, Rail On, Kaokokokorobo.

Pia aliwahi kushirikishwa na bendi za vijana kama Mashujaa band katika wimbo wa Umeninyima. Kwa upande wa hapa Tanzania aliwahi kuimba na msanii maarufu hapa nchini Diamond Platnumz katika kibao cha Chacun Pour Soi.

Moja ya kadhia ambayo aliwahi kupitia enzi za uhai wake ni pamoja na kukamatwa kwa madai ya ulanguzi wa binadamu.

Tarehe 18 Februari 2003 maafisa wa idara ya upelelezi nchini Ufaransa walimkamata Papa Wemba kwa tuhuma za kuwaingiza raia wa Zaire (kama ilivyoitwa wakati huo) barani ulaya kinyume cha sheria.

Mahakama ya ubelgiji ilimpata na hatia mwezi Juni mwaka wa 2003 na ikamhukumu kifungo cha mwaka mmoja na miezi mitatu jela. Aidha mahakama hiyo ya Brussels ilimpiga faini ya euro 22,000, ambapo hata hivyo alitumikia kifungo cha miezi mitatu na nusu gerezani baada ya mdhamini wake kulipia dhamana ya Euro €30,000.

Alipoachiwa huru aliwaambia mashabiki wake kuwa aliyokumbana nayo akiwa gerezani yamemfunza mengi sana.

Katika utunzi wa wimbo wake Numéro d’écrou (2003) Papa Wemba anasimulia kukutana na mwenyezi Mungu akiwa gerezani.

Kifo Chake:

Video inayosambazwa katika mitandao ya kijamii ilimuonesha Papa Wemba akiwa jukwaani akiendelea na ya uimbaji kisha akaonekana akianguka ghafla jukwaani.

Wanabendi wake waliokuwa jukwaani mjini Abidjan Ivory Coast katika tamasha la muziki la Femua waliendelea kupiga densi kabla ya mmoja wao kukimbia kumuokoa baada ya kuona amesalia chini kwa sekunde kadhaa akiwa anatetemeka.

Msemaji wa Papa Wemba Henry Christmas Mbuta Vokia aliiambia Radio Okapi kuwa Marehemu Papa Wemba alikuwa ameingia muda mchache tu jukwaani kisha akacheza wimbo wa kwanza, mashabiki wakamuomba awaimbie tena wimbo mwengine akakubali, lakini dakika chache tu baada ya kuanza kupiga wimbo wake wa tatu, Papa Wemba alianguka na kuzirai ghafla jukwaani.

Msemaji huyo aliongeza kwa kusema Watu wa shirika la msalaba mwekundu walijaribu kumsaidia lakini hakuonesha dalili nzuri na hivyo wakampeleka hospitalini kwa dharura lakini baada ya dakika karibu thelathini hivi wakaambiwa kuwa Papa Wemba ameaga dunia.

Inasemekana kuwa Enzi za uhai wake aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa anapenda sana muziki na anapenda hata siku akifariki dunia mauti yamkute akiwa kwenye kazi yake ya muziki, na kweli ndoto yake alitimia. Taarifa nyinginge hudai kwamba kifo chake kilitokana na kuwekewa sumu kwenye ‘microphone’.

Papa Wemba alikonga nyoyo za wapenzi wa muziki wa Soukus nchini DRC na kote duniani kwa kipaji chake cha kipekee na sauti isiyokuwa na mfano ambayo mpaka sasa haijawahi kupata mbadala wake.  Alikuwa ni mtunzi, mweledi wa kuimba, kucheza ala za muziki na pia kusakata rhumba yaani kunengua kiuno.

About Muhammed Khamis

hosearevocatus9@gmail.com

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *