habari

Balozi Seif ataka maeneo ya historia kutunzwa

on

Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amesema wananchi wanapaswa kujua historia yao ili kulinda uhuru wao, heshima, utamaduni na mazingira yao yanayowazunguuka.

Alisema binaadamu asiyejua historia yake ni sawa na mtumwa wakati wote akiendelea kutawaliwa kifikra jambo ambalo ni hatari katika  maisha yake.

Alisema hayo alipofanya ziara fupi ya kukagua mahandaki mawili ya Mangapwani yaliyokuwa yakitumika kuhifadhia watumwa ambayo kwa sasa yamekuwa sehemu muhimu ya kujifunza historia ya biashara hiyo iliyopigwa marufuku tokea karne ya 18.

Alisema Zanzibar ilikuwa kituo muhimu cha historia iliyounganisha sehemu nyingi duniani, hivyo Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale, ina jukumu la kusimamia maeneo yote muhimu ili wageni na wananchi wapate fursa ya kujifunza.

Aliwakumbusha vijana wanaosimamia maeneo hayo kufanya jitihada ya kujifunza historia ili kuepuka tabia ya kutoa taarifa zisizo za kweli kwa wageni.

Msimamizi wa mahandaki ya Mangapwani, Makame Omar Said, alisema maumbile ya eneo hilo muda wote yamekuwa ya kujificha kutokana na hali halisi ya biashara yenyewe ilivyokuwa ikifanywa.

Alisema utafiti unaonyesha kwamba bado idadi ya wazawa wanafika eneo hilo kujifunza historia ni ndogo ikilinganishwa na wageni.

 

Aliyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni mahandaki ya Mangapwani, msikiti mkongwe wa Kizimkazi, mji wa makutani uliopo katika kisiwa cha Tumbatu na mji wa Mwinyimkuu uliopo Dunga.

Alisema mahandaki ya Mangapwani yana bahati ya kutembelewa na wageni wengi, watalii, wanafunzi na watafiti ikilinganishwa na sehemu nyengine za kihistoria zilizopo Zanzibar.

Akielezea changamoto zinayoyakabili maeneo ya kihistoria nchini, Mkuu wa wilaya ya kaskazini ‘B’, Rajab Ali Rajab, alimueleza Balozi Seif kwamba  uhaba wa wafanyakazi ni tatizo linalopaswa kuangaliwa na serikali.

Zanzibar iliyokuwa kituo cha biashara ya utumwa katika mwambao wa Afrika Mashariki, ilisimamisha chini ya utawala wa Uingereza mwaka 1873.

About Muhammed Khamis

hosearevocatus9@gmail.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *