habari

Dkt. Ndugulile: “Tumetengeneza Mikakati Jumuishi Kati Ya Ugonjwa Wa TB Na UKIMWI”.

on

Katika mikakati yake ya kuwatambua wagonjwa wanaoishi na virusi vya UKIMWI pamoja na TB, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto imesema Imeazimia kutembea maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi ikiwemo baa, migodini na mahali pengine ili waweze kuwatambua waathirika kiurahisi.
Naibu Waziri wa Wizara hiyo Dkt. Faustine Ndugulile, amesema hayo leo Aprili 23, 2018 Bungeni mjini Dodoma katika kikao cha 15 mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akijibu la nyongeza kutoka kwa Mbunge Masoud Abdallah aliyetaka kufahamu serikali ina mikakati gani katika kutoa elimu maalum ambayo itaweza kuenea kwa kasi zaidi katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi zaidi.

“Serikali baada ya kuona kumekuwa na changamoto kubwa sana katika utambuzi wa makundi maalum ambayo wengi wamekuwa wakiathirika na ugonjwa wa TB na UKIMWI. Hivyo tumeamua kujielekeza kutoa elimu kwa njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari lakini vilevile tuna mkakati mahususi wa kuwatafuta wagonjwa wa TB katika migodi sambamba na hilo tumetengeneza mikakati jumuishi kati ya ugonjwa wa TB na UKIMWI”, amesema Dkt. Ndugulile.

Dkt. Ndugulile ameendelea kwa kusema wizara hiyo imeanza kujielekeza mahali kwenye watu wengi ili kuweza kuwapata kwa pamoja hususani wanaume ambapo mara nyingi wanakuwa katika bar. “Msishangae kutuona na sisi tunapita huko kuwaomba kufanya upimaji wa suala la ugonjwa wa UKIMWI pamoja na TB”.

Aidha, Dkt. Ndugulile amesema njia kuu ya kupambana na kulishinda tatizo la kifua kikuu , ni pamoja na kumgundua mgonjwa wa TB mapema na kumuweka katika matibabu, na kwamba ndio jambo ambalo lipo kwenye mikakati ya serikali katika kufufua uwezo wa kufikia watu wote wanaohitaji huduma za TB ili kuwagundua mapema na kuwatibu kikamilifu.

About Muhammed Khamis

hosearevocatus9@gmail.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *