habari

Fatma Karume Ashinda Urais TLS. Sasa Kurithi Mikoba Ya Tundu Lissu.

on

Wakili wa kujitegemea, Fatma Karume amechaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (Tanganyika Lawyers Society – TLS), akichukua mikoba ya aliyekuwa Rais wa Chama hicho, Tundu Lissu baada ya muda wake kumalizika. Katika uchaguzi uliofanyika Jumamosi hii April 14 2018, Jijini Arusha, Dkt. Rugemeleza Nshala amechaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa chama hicho huku Ndugu Omar Shaaban akichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar Lawyers Society (ZLS).

Uongozi wa TLS hudumu kwa kipindi cha mwaka mmoja tu, na baada ya hapo viongozi wengine huchaguliwa, hii ikiwa ni kwa mujibu wa katiba ya Chama hicho,

Aidha, katika hatua nyingine Kamati ya Chama cha Wanasheria wa Tanganyika, (TLS) iliyoundwa kujadili uamuzi wa Mwanasheria wa Mkuu wa Serikali (AG) wa kuzifanyia mabadiliko kanuni za uchaguzi wa chama hicho imesema, AG hakuwa na mamlaka ya kufanya mabadiliko yoyote

Godwin Ngwilimi Makamu wa Rais wa TLS ambaye amemaliza muda wake, ametoa hoja hiyo na kumtaka mjumbe wa Baraza la uongozi, Jeremiah Mtobesya kusoma mapendekezo hayo ambayo yalisema Mwanasheria Mkuu wa serikali hakuwa na Mamlaka ya kufanya mabadiliko bali kuyachapisha kwenye gazeti la serikali.

Pia walipendekeza kufuata njia za kiutawala kuonana na Mwanasheria Mkuu au kwenda mahakamani kutafuta tafsiri ya mamlaka yake kwa TLS.

Fatma Karume amesema maboresho yaliyofanywa hayana msingi wa kisheria kwa kuwa kanuni za uchaguzi wa TLS zinaanza kufanya kazi mara tu baada ya kupitishwa na mkutano mkuu. Hata hivyo wajumbe hao walikubaliana na baraza la uongozi kutengeneza kanuni ambazo zitatamka kuwa si lazima zitangazwe kwenye gazeti la serikali ili ziwe halali.

About Hosea Revocatus

hosearevocatus9@gmail.com

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *