We have 298 guests and no members online

Tukumbushane Tulikotoka: Ndani Ya Miaka Kumi, Nyerere Alituvusha Kwenye Mitihani Migumu Mitano, Na Hakuwa Dikteta...

Image may contain: 1 person, standing, walking, shoes and outdoor

 

Ndugu zangu,

Historia ni Mwalimu mzuri. Na tuamini, kuwa ili mwanadamu ajue mahali alipo na anakokwenda, ni muhimu awe na uelewa wa alikotoka. Aijue historia yake ili imsaidie kwenye kujitambua.

Nilipata kuyaandika haya kufuatia mada niliyoianzisha juu ya hamu inayojengeka kwenye jamii ya kutamani udikteta.

Nilimjibu mjumbe wangu ndugu Galinoma kama ifuatavyo;

"Galinoma, foleni za unga haikumaanisha udikteta. Dunia ilikuwa tofauti na sasa. Dunia ilikuwa kwenye vita baridi na mapambano ya kiitikadi; Ujamaa dhidi ya Ubepari. Mimi ni Mjamaa, na zaidi ni Social Democrat.

Nimekulia katikati ya mapambano hayo ya kiitikadi. Nchi yetu huo ilipitia mitihani migumu mitano kama taifa; Mtihani wa kwanza; migogoro miwili ya mafuta duniani.

Ni kati ya 70 na 73. Mtihani wa kwanza wa mafuta ni mwaka 1970. Wa pili mwaka 1973. Mtihani wa tatu ni ukame wa mwaka 74. Watanzania tulikula 'Unga wa Yanga' kwa maana ya unga wa njano. Mtihani wa nne ni kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977. Mtihani wa tano ni Vita vya Kagera 1978-79.

Ikumbukwe hapa, kuwa Julius Nyerere akiwa hajatimiza hata umri wa miaka hamsini, alikabidhiwa Tanganyika iliyokuwa na wasomi wasiojaa kiganjani. Ukweli wasomi wa nchi hii walijulikana kwa majina. Madaktari bingwa wa tiba ilikuwa shida kuwataja wakafika sita. Kimsingi nchi ilianza kama na wasomi  9 tu wenye majina. Ni watu wa aina ya  George Kahama, Injinia Gabriel Kimbuzi, huyu ndio alikuwa Mechanical Engeneer wa kwanza Tanganyika. Kwenye tiba tulikuwa na madaktari aina ya  Dr Mwaisela, kumbukumbu yake ni Wodi ile ya Wagonjwa pale Muhimbili. Kulikuwa na  Dr. Pim,  Dr. Mtawali,  Dr Shaba na Dr Hartman. Wasomi wengine walioshika ukurugenzi wa mashirika ni watu wa aina ya Dustan Omar. Huyu alikuwa  Director General wa East Africa Postal And Telecommunications. Kulikuwa na msomi Joseph Kasella Bantu na wengineo wachache tunawasoma kwenye vitabu. 

Si ajabu basi, katika kuwatafuta Ma-DC wa kuwateua, Julius Nyerere ilibidi afikie  hata kuwachomoa kwenye sukani zao, Wana-TANU waliokuwa madereva wa Teksi Mjini. Hawa kwa vile lugha ilipanda kidogo na mambo ya kimjini mjini wanayajua ikiwamo kuongea na kumwaga sera za TANU, basi, wakapewa Wilaya wakawe Ma- Area Commissioner, kama ilivyojulikana wakati huo .  

Ndio,  mwaka 1968 nchi ilihitaji Wahasibu 1500, lakini wahasibu  waliokuwa wana-graduate  hawakujaa kiganjani. Ndio hapo Julius Nyerere akaelekeza kuanzishwa  vyuo vya Uhasibu kama vile DSA. Idadi yake vikafikia vitatu nchi nzima.

Julius Nyerere ameondoka madarakani mwaka 1985 nchi ikiwa ina uwezo wa kuzalisha wataalamu wasomi kwenye sekta zote muhimu. Si hivyo tu, nchi ikiwa na uwezo wa kuwa na watalaamu wake wa masuala ya nyuklia na na makombora ya atomic. Ni watu wa aina ya Dr Ghalib Bilal aliyepata kuwa Makamu wa Rais pia.

Naam, ndani ya miaka kumi nchi yetu ilipitia mitihani migumu mitano. Nilikuwa na miaka kumi na moja pale Kinondoni Biafra, nilipomsikia kupitia redio, Julius Nyerere akitangaza vita dhidi ya dikteta Idd Amin. Ni Idd Amin aliyetuvamia na kuchukua sehemu ya ardhi yetu.

Usiku ule niliyaona magari ya kijeshi yakipita nje ya nyumba yetu. Ni  pale Morocco road,  Kinondoni Biafra. Umeme ulikatwa, magari yale yalikuwa yakitokea kambi ya Lugalo kwenda mpakani.

Ndio, nimeishi na kushuhudia kwa macho yangu mwaka ule wa 1979, pale uwanja wa taifa, mbali ya kumpoteza rubani wetu kwenye ndege ya kivita iliyokuwa ituangukie uwanjani, lakini,  rubani yule akajitahidi aende akaanguke nayo nje ya uwanja. Nakumbuka Julius Nyerere alibaki amekaa akiwa amekunja miguu na kushika tama. Alionekana kutulia.

Na ilipofika muda wa kuhutubia, Julius alitoa hotuba muhimu yenye kutuandama hadi leo. Aliamua kuacha kuzungumzia ajali ile, bali, alirudia kusema.  kuwa vita si lelemama, na kwamba Watanzania tujiandae kufunga mikanda kwa miezi kumi na nane. Na hakika,  imekuwa zaidi ya miaka 18, na hadi leo tuna makovu ya vita vile . Ni makovu ya kiuchumi.

Ni ukweli wa kihistoria, kuwa  ndani ya miaka kumi nchi yetu ilipitia mitihani hiyo mitano na migumu kuwahi kutokea. Nyerere hakuwa dikteta, alijenga uongozi wa kitaifa uliojenga ushawishi na mshikamano wa kitaifa tukaweza, hata kwa tabu, kuvuka mitihani hiyo mitano na tukabaki salama kama taifa.

Bila shaka yeyote, pamoja na mapungufu yake ya kibinadamu. Mazuri ya Julius Nyerere yamezidi mapungufu hayo. Julius Nyerere alikuwa na atabaki kuwa Shujaaa wa Taifa Hili.

 

Maggid Mjengwa.

Tuma Maoni


Security code


Anzisha upya


Karibu Mjengwablog

Tafuta Habari

Nafasi za Kazi & Masomo

Prev Next

We are Hiring - Senior Web / Mobile Deve…

As we are expanding our operations , W...

Soma zaidi

Job Vacancy: Business Administrative Ass…

The primary role of the business admin...

Soma zaidi

JOB: Sales and Marketing person for sell…

BANIZ SAFARI is one of the project ava...

Soma zaidi

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI JUU YA AJI…

  Jumla ya Walimu wapya 36,021 a...

Soma zaidi

Nafasi za kazi - Web Developers

We are looking for a talented web deve...

Soma zaidi

Video Gallery

Kwa video za matukio mbalimbali yanoyotokea Tanzania.

bshyera11_ba222.jpg

Smartads

 

Maoni ya Watembeleaji

BLOG SHABIHANA