habari

Hatimaye Puigdemont Atiwa Nguvuni Ujerumani.

on

Msemaji wa Polisi wa kituo cha Schleswig-Holstein nchini Ujerumani amethibitisha kukamatwa kwa rais wa zamani wa eneo la Catalonia Carles Puigdemont maajira ya 11:19 asubuhi, wakati alipojaribu kuvuka mpaka kwa kutumia gari akitokea nchini Denmark na kwamba kukamatwa kwake kumetokana na hati ya kukamatwa kwake iliyotolewa kwenye nchi za Ulaya.

Msemaji huyo wa polisi ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kuwa Puigdemont kwa sasa yuko kizuizini akisubiri taratibu zaidi.

Msemaji wa chama cha Puigdemont Anna Grabalosa kwa nyakati tofauti nae amethibitisha kukamatwa kwa kiongozi wao na kudai kuwa alikamatwa akiwasili nchini Ujerimani akitokea Denmark.

“Imetokea wakati akivuka mpaka wa Ujerumani na Denmark, baada ya kukamatwa alihudumiwa vizuri na wanasheria wake wote wamefika, hiko ndicho nachoweza kusema kwa sasa,” alisema msemaji wa chama cha Puigdemont.

Puigdemont anatakiwa nchini Uhispania kujibu mashtaka ya kufanya uasi na kuichafua Serikali kutokana na uamuzi wake wa kutaka eneo la Catalonia kujitenga.

Kabla ya kukamatwa kwake alitembelea nchi ya Finland tangu siku ya Alhamisi lakini akafanikiwa kuwakimbia polisi wa nchi hiyo muda mfupi baada ya kupata taarifa za kuwa anatakiwa kukamatwa.

Wakili wa Puigdemont, Jaume Alonso-Cuevillas amesema kupitia mtandao wake wa kijamii wa twitter kuwa Puigdemont alikamatwa na polisi wa Ujerumani wakati akisafiri kurejea nchini Ubelgiji ambako amekuwa akiishi tangu akimbie nchi yake.

Mpaka sasa haijafahamika ikiwa ni lini polisi ya Ujerumani itamsafirisha Puigdemont kwenda nchini Uhispania.

About Muhammed Khamis

hosearevocatus9@gmail.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *