We have 134 guests and no members online

‘Kuna Binadamu Ambao, Kwa Kujali Fedha Wanauza Sumu Kwa Binadamu Wenzao’

Posted On Monday, 24 December 2012 20:03 Written by M Mjengwa
Rate this item
(0 votes)

‘Kuna Binadamu Ambao, Kwa Kujali Fedha Wanauza Sumu Kwa Binadamu Wenzao’\

Na: Meshack Maganga-Iringa.

Ndugu zangu,

Dhumuni la wewe na mimi kuwepo duniani ni kuishi maisha yenye madhumuni, maisha yenye mafanikio na maisha yanayonufaisha wengine. Wanadamu wote walioweza kufanikiwa kwa kujitengenezea mafanikio wenyewe kutoka chini ni wale ambao wametambua sababu ya wao kuwa wao, wanajua ni nini wao na wenzao wanakitaka na wanajua kuwa ili maisha yao yawe na maana lazima wafanikiwe katika hilo.Ukitaka kutengeneza maisha yenye mafanikio duniani, tafuta kujua dhumuni lako hapa duniani.

Ndoto kwenye maisha yetu ni malengo yetu ya kuwa hapa duniani. Kutafakari na kuwa na vusheni kwa nini mtu yuko hapa duniani na jindi mtu anavyojiambia kuhusu anachoamini ndilo lengo lake la kuwepo hapa duniani. Lakini kwa bahati mbaya wengi wetu hatujui malengo yetu, kama tulivyokeisha sema hapo awali.

 

Mwalimu wangu wa Chuo kikuu, Dr. Mark Fihavango katika kitabu chake cha ‘Tumpate Wapi Mtu Huyu’ amemunukuu mwandishi maarufu duniani Steve Covey kwenye kitabu cha 'The 7 Habits of Highly Effective People', anasema ni vizuri kama mtu anataka kujua ndoto yake au lengo la kuletwa kwake hapa duniani akaanza kwa kujipiga picha kwamba yuko kwenye mazishi yake mwenyewe.

 

Hebu jaribu kufikiria kwamba mwili wako uko ndani ya sanduku au jeneza ukiwa umewekwa juu ya lundo la mchanga kando ya kaburi , tayari kwa kuzikwa. Halafu jaribu kuwaweka pichani wale waliokuwa karibu nawe ambao wanasoma historia ya maisha yako.

 

Hebu jaribu kwenda ndani na kuyafikiria yale ambayo yanasemwa kwenye risala hiyo kuhusu maisha yako hapa duniani na mchango wako. Je, ungependa kusikia maneno gani kutoka kwenye risala hiyo? Hebu piga picha ya watu wote ambao wanakufahamu wanavyosema kuhusu kifo chako, wakiwa majumbani mwao au kwingine. Ungependa kusikia wakikuzungumzia vipi?

Halafu rudi kwenye kufikiri kwako kwa kawaida, yakague maisha yako na kujiuliza kama unavyoishi sasa na unayoyafanya ndiyo ambayo ungejisikia vizuri kusikia yakisemwa kukuhusu baada ya kufa kwako.

 

 

Bila shaka unaweza kugundua kwamba, ungependa kufanya mambo Fulani maishani mwako, bila shaka ungegundua ambalo au ambayo hujayafanya na ungependa sana kufanya kabla jujaondoka duniani. Je, hizo au hayo hayawezi kuwa ndiyo ndoto yako?

 

Sisi kama binadamu tunajipenda na hakuna awezaye kulizuia jambo hili. Lakini kujipenda kwa ziada kunaweza kuzuilika kama mtu atamua. Kujipenda kwa ziada ndiko ambako kunapelekea dunia kuwa kama ilivyo leo kwa upande wa uharibifu.

 

Yale yote ambayo hayakwenda sawa kufuatana na mpango wa Mungu yamesababishwa na uziada wa kujipenda kwa binadamu, Mpango wa Mungu ni kuwa na dunia ambayo haina makovu walavidonda. Lakini dunia hii tunamoishi imejaa vidonda na makovu zaidi kuliko uzima. Vidonda na makovu haya, kama ambavyo tumesema ni matokeo ya binadamu kujipenda kupita kiasi, kujipenda ambako kunamfanya adhani kwamba yeye anastahili zaidi kuliko mwingine na kumemfanya awe pia mvivu wa kufikiri.

 

Ni binadamu wachache sana ambao wako tayari kukaa chini na kujiuliza kama kweli wana tofauti nawengine. Ni wachache kwa sababu kila mmoja anaamini kwamba ni tofauti na mwingine, iwe ni kwa mwenye mali au asio nayo, iwe ni kwa mwanamke au mwanamume, au kwa msomi na asiyesoma, kila mmoja anaamini kwamba ana tofauti na mwingine. Anashindwa binadamu kujua kwamba, yeye kama binadamu hana tofauti na ninadamu mwingine.

 

Labda tukumbushane kwamba binadamu hawi binadamu kwa sababu ana magari makubwa mia moja au ana nyumba za fahari mji mzima, lakini pia hawi binadamu kwa sababu anashinda na kulala na njaa au anatembea makalio yakiwa nje kwa ulitima (umasikini). Binadamu anakuwa binadamu kwa sababu kuna sifa ambazo hupatikana kwaki na kwa mwingine bila kujali huyo mwingine yukoje kimwili na kihali.

 

Kushindwa huku ndiko ambako huwafanya binadamu kuwapa wenzao kile ambacho kama wangepewa wao kungezuka balaa kubwa. Binadamu wamekuwa wakijaribu kuridhisha miili yao na pengine nafsi kama siyo tama zao kwa kuwafinyia wengine lile ambalo kwao lingekuwa ni gumu sana kulivumilia.

 

Leo hii kuna binadamu ambao kwa kujali fedha wanauza sumu kwa binadamu wenzao. Kwa kutaka fedha huuza vyakula ambavyo wanajua wazi kwamba, vitadhuru afya za wengine na kuwauwa. Wanauza vyakula hivyo wakiwa na uhakika kwamba, baada ya muda fulani, hao waliouziwa wataugua kansa au maradhi mengine hadi kufa. Lakini ni wazi wao wasingekubali kufanyiwa jambo hilo.

 

Kuna wale ambao kwa matumizi ya vyeo vyao huwakosesha wengine haki zao kwa sababu tu wengine hao hawana nguvu na uwezo wa kupambana nao. Hawa kwa makusudi huwafanya watu wengi kuishi katika ulitima wa kudumu wakati wangeweza kuinuka na kuishi kama wao.

 

Kuna kundi kubwa la binadamu ambalo kamwe halijawahi kufanya jema kwa wengine, halijawahi kutamka jema kwa wengine na halijawahi kufikiria jema kwa wengine. Kundi hili lina watu ambao wao kila siku wanafikiria ni kwa namna gani watatumia ujinga wa wengine kwa manufaa yao, ujinga wa wengine kwa kujipatia ziada na “kutanua” huku wengine hao wakiporomoka na kuingia kwenye shimo la kiza cha ukosefu na majuto.

 

Umefika wakati ambapo inabidi tuanze kuheshimu nguvu za maumbile, inabidi tuanze kuheshimu ubinadamu katika ujumla wake. Inabidi tujue kwamba kinachotufanya tusimame leo na kujidai, kujivuna na kujiona tu bora sana ni kwa sababu kuna binadamu wengine wanaotuzunguka. Kinachotufanya leo na kujidai, kujivuna na kujiona tu bora sana ni kwa sababu kuna binadamu wengine wanaotuzunguka.

 

Kinachotufanya leo hii tutamani kuonekena wakubwa zaidi, wenye uwezo zaidi na wenye heshima zaidi ni kuwepo kwa binadamu wengine, kuwepo kwa wenzetu. Kwa hiyo, sisi siyo binadamu hata kidogo kama tunavyodhani, bila binadamu wengine kuwepo.

 

Mbaya zaidi ni kwamba, sisi siyo binadamu kamili kama wenzetu siyo kamili. Ukamilifu wao ndiyo unaotupa sisi ukamilifu. Ukitaka kuthibitisha jambo hili unaweza, kwani ni rahisi sana.

 

Hebu anza sasa kutenda yale ambayo hata wewe ungependa kutendwa na kuacha kuwatenda wengine yale ambayo hata wewe usingependa kutendewa. Nina uhakika baada ya muda Fulani utagundua ukweli Fulani na bila shaka utawasiliana nasi kutufahamisha. Hutapoteza chochote kufanya jaribio hilo bila shaka.

 

 

meshackmaganga@gmail.com

Read 4202 times

Add comment


Security code
Refresh

Tafuta Habari

Blog Shabihana

Maji