We have 146 guests and no members online

Wizara yapokea mrejesho wa mradi wa afya ya uzazi wa Thamini Uhai na namna inavyoongeza matumizi ya vituo vya afya na kuokoa maisha

Posted On Thursday, 16 February 2017 07:00 Written by
Rate this item
(0 votes)

Wadau kutoka shirika la Thamini Uhai, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Ofisi ya Rais - Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa wakimsikiliza kwa makini Waziri Ummy Mwalimu wakati wa mkutano wa mrejesho wa shirika la Thamini Uhai, jijini Dar-es-Salaam Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto - Mh Ummy Mwalimu (katikati) na Dr Hussein Kidanto - kaimu mkurugenzi wa idara ya huduma za kinga Wizara ya Afya (kushoto) wakishauriana  na Mkurugenzi mtendaji wa Thamini Uhai, Dr Nguke Mwakatundu (Kulia) wakati wa mkutano wa mrejesho wa shirika la Thamini Uhai, jijini Dar-es-Salaam

Wadau kutoka shirika la Thamini Uhai, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Ofisi ya Rais - Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa wakishauriana wakati wa mkutano wa mrejesho wa shirika la Thamini Uhai, jijini Dar-es-Salaam

Tokea 2008, Thamini Uhai imesaidia vituo vya huduma za afya 19 na zahanati 18 katika mikoa mitatu, na hivyo kujenga mfumo utakaokuwa mfano bora na inayoweza kutumika kokote nchini kuokoa maisha ya akina mama na watoto wachanga.

(Februari 15, 2017, Dar es Salaam, Tanzania) – Leo jijini Dar-es-Salaam, Thamini Uhai imetoa mrejesho wa shughuli zake tokea kuanzishwa kwake na kuwasilisha mipango yake kwa mwaka 2017 kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Thamini Uhai (iliyoitwa World Lung Foundation hapo awali), imefanya kazi kwa karibu na wahisani pamoja na serikali za mikoa, kujenga mfumo ambao umepelekea ugatuzi wa huduma za dharura za kuokoa maisha ya mama na watoto wachanga kutoka hospitali kwenda kwenye vituo vya afya. Mfumo huu wa kipekee wa huduma ya afya umehusisha pia kuboresha vituo vya huduma za afya ili viweze kutoa huduma hizi za dharura, kuendeleza mafunzo ya jamii kupitia vyombo vya habari na waelimishaji jamii ili kuhamasisha jamii itumie vituo vya huduma za afya, kuboresha mifumo ya rufaa, kuhakikisha upatikanaji wa ushauri wa afya kila wakati. Pia shirika imetoa mafunzo, usimamizi na elimu endelevu kwa wahudumu wa afya, waganga wasaidizi (AMO) na manesi ambapo elimu hiyo inatolewa na madaktari bingwa ili kugatua huduma na ujuzi na hivyo kuongeza uwezo katika jamii zilizopo pemebezoni.

Akizungumzia mafanikio yao, Dr. Nguke Mwakatundu, Mkurugenzi Mtendaji wa Thamini Uhai,  amesema:

“Moja ya mafanikio yetu muhimu ni jinsi shughuli zetu zimeweza kuleta mabadiliko katika maisha ya wagonjwa katika nyanja zinayotuhusu. Tumeona vifo vya uzazi na rufaa zikipungua kwa kiasi kikubwa na kwa njia endelevu katika maeneo haya, pamoja na kuona ongezeko la maana katika idadi ya wanawake wanaoamua kujifungua katika vituo vya huduma za afya.”

Akitilia mkazo baadhi ya changamoto, Dr. Mwakatundu ameeleza kuwa ili mafanikio haya yawe endelevu kuna haja ya kupanga rasilimali za kutosha kwa ajili ya wafanyakazi wa afya na kuboresha mfumo wa usamabazaji wa vifaa na madawa.

Waziri wa Afya, Mh, Ummy Mwalimu akitoa mchango wake kuhusu kazi za Thamini Uhai, amesema: “Ningependa kutambua mchango wenu katika kuhakikisha akina mama wanajifungua kwa usalama katika mikoa husika. Naelewa kuwa mmefanya kazi kubwa kuboresha mifumo ya huduma za dharura katika vituo vya afya na hospitali, mmeanzisha kampeni za mawasiliano na kuimarisha mifumo ya rufaa kutoka vituo vya afya kwenda hospitali.”

Thamini Uhai imekwisha kabidhi serikalini shughuli zake za mradi wa afya ya uzazi katika mikoa miwili – Morogoro na Pwani, na imepanga mwaka 2017 kuanza utaratibu wa kukabidhi shughuli zake katika mkoa wa Kigoma.

Kuhusu Thamini Uhai

Tangu mwaka 2008, Thamini Uhai (zamani iliyojulikana kama World Lung Foundation Tanzania) imefanya kazi ili kusaidia kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga na kuboresha upatikanaji wa huduma bora za uzazi wa dharura (CEmONC) katika jamii, hasa katika maeneo ya vijijini na sehemu zilizo pembezoni ambapo wagonjwa awali walikuwa wanasafiri masaa tatu au nne kwenda hospitali ya karibu. Mpango mkakati wetu ni kusaidia mawasiliano bunifu na kampeni za  jamii ili kuongeza matumizi ya vituo vya afya na uzazi wa mpango; kuboresha miundombinu; na kutoa mafunzo na kusaidia kliniki zisizo na daktari kutoa huduma ya uzazi wa dharura. Kwa mikoa Kigoma, Morogoro, na Pwani:

  • Thamini Uhai imeboresha kikamilifu, kukarabati au kujenga upya vituo vya afya 15 vijijini na hospitali za wilaya na inasaidia vituo 5 zaidi. Pia inasaidia zahanati 18 katika maeneo ya vyanzo vya maji, kuboresha upatikanaji wa mahudhurio ya uzalishaji wenye ujuzi kwa ubora wa juu na huduma za uzazi wa dharura na watoto wachanga.
  • Zaidi ya wasaidizi 100, waganga wasaidizi, nesi-wakunga, na maafisa wa kliniki wamepata mafunzo ya kina kuhusu huduma ya uzazi wa dharura au nusu kaputi.
  • Matumizi ya kituo cha afya kwa ajili ya uzalishaji yameongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka wanawake 21,661 waliojifungua katika vituo vinavyoungwa mkono mwaka 2011, hadi wanawake 26,189 waliojifungua mwaka 2015.

Mpango huu umepokea msaada wa kifedha kutoka Bloomberg Philanthropies, Blue Lantern, Fondation H & B Agerup, na Svenska Postkod Stiftelsen na Thamini Uhai ni mshirika wa Vital Strategies.

Kwa maelezo zaidi tembelea tovuti: www.thaminiuhai.or.tz or Twitter @ThaminiUhai, or Facebookhttps://www.facebook.com/ThaminiUhai/

Maria Sarungi-Tsehai, msarungi-tsehai@vitalstrategies.org, +255 784235215

Kuhusu Vital Strategies

Vital Strategies ni shirika la kimataifa linalojishughulisha na masuala ya afya na linalenga kusaidia kuongeza kasi ya maendeleo katika kupambana na magonjwa yenye athari kubwa duniani.

Timu yetu inatumia mikakati iliyojikita katika ushahidi  na uvumbuzi ili kubuni na kutekeleza sera nzuri za afya ya umma, kusimamia mipango kwa ufanisi, kuimarisha mifumo ya data, kufanya utafiti, na kubuni kampeni ya kimkakati ya mawasiliano kwa ajili ya sera na mabadiliko ya tabia.

Kwa taarifa zaidi au kupanga mahojiano na mtaalam wa afya ya jamii au afya ya uzazi kutoka Vital Strategies, tafadhali wasiliana na Tracey Johnston, Vital Strategies, at +44.7889.081.170 autjohnston@vitalstrategies.org

Read 441 times

Add comment


Security code
Refresh

Tafuta Habari

Blog Shabihana

Watumishi