We have 214 guests and no members online

Muhingo Rweyemamu Niliyemfahamu...

Posted On Monday, 04 September 2017 05:22 Written by
Rate this item
(0 votes)

Image may contain: 1 personNdugu zangu, 

Ametutoka, Muhingo Rweyemamu. Kila nilipokutana nae nilizoea kumwita Kaka.

Nilifahamiana na Muhingo kupitia ndugu yangu Absalom Kibanda. Nakumbuka jioni moja mwaka 1996 giza likianza kuingia nyumbani kwetu Kinondoni Biafra , alikuja Absalom Kibanda. 

Nikakaa nae sebuleni. Kibanda akaliweka gazeti la Mwananchi mezani. Kisha akatamka;

" Braza niko na Muhingo tunaomba uanze kutuandikia makala kwenye gazeti hilo tunaloliongoza."

Nilimkubalia Kibanda na hazikupita siku mbili akanikutanisha na Muhingo Rweyemamu pale kwenye ofisi zao, Jengo la CCM Kariakoo.

Muhingo alinichangamkia sana na akaniahidi ushirikiano. Tangu hapo tukaanza kufahamiana zaidi.

Nakumbuka mwaka 2003 nilipata bahati ya kupanda basi moja na Muhingo kuanzia Ubungo kwenda Iringa. Ni basi la Scandinavia. Naweza kabisa kusema, kwenye safari ile ndipo niliweza kumfahamu zaidi Muhingo.

Safari ile ya saa tisa barabarani ilikuwa darasa kubwa na muhimu kwangu. Wakati huo nilikuja likizo nikitokea Sweden. Muhingo aliweza kunieleza mengi anayoyaona na anavyoyatafsiri kupitia uandishi. Muhingo alionyesha kuwa na uelewa mkubwa wa masuala ya nchi hii hata yale yasioandikwa magazetini.

Mahali fulani kwenye mazungumzo yetu tukaingia kwenye mgogoro wa DR Congo. Muhingo tena akaonyesha alivyo na uelewa mpana wa Nchi za Maziwa Makuu na migogoro yake.

Mathalan, alinisimulia safari yake ya kiuandishi kupitia Rwanda hadi Goma akiwa nyuma ya vikosi vya Laurent Kabila. Alinieleza jinsi askari wale walivyowafuata milimani wanajeshi wa Maimai. Milio ya bunduki na mabomu ilikuwa ni kitu cha kawaida na akazoea. Akanithibitishia pia kuwa askari wa Kagame nao waliokuwepo kwenye operesheni ile ndani ya DRC.

Tukafika Iringa kwa basi kwenye safari niliyoiona fupi sana kutokana na mazungumzo yangu na Muhingo.

Jioni ile nikiwa Iringa, Muhingo aliyekuwa, wakati huo, Mwanafunzi wa Tumaini University, alihakikisha nafika anakoishi pale maeneo ya Semtema. 

Nilipofika Semtema, kwenye nyumba ndogo aliyokuwa akiishi Muhingo, aliishi pia ndugu yangu Assah Mwambene. Naye alikuwa mwanafunzi wa Tumaini University.

Mazungumzo yaliendelea tukiwa watatu kwenye familia ya habari.
Chakula kikapikwa, tukala. Tukaendelea na mazungumzo kuhusu masuala mbali mbali ikiwamo media na demokrasia. Tuliongea hadi usiku mwingi. 

Kesho yake Muhingo alinialika kutembelea Tumaini University. Nilipofika Chuoni ndipo nilipoona namna Muhingo alivyoheshimika kuanzia kwa wanafunzi wenzake hadi wahadhiri wa chuo.

Muhingo alikuwa Waziri wa Habari na Utangazaji kwenye Serikali ya Wanafunzi. Kwa nafasi yake hiyo alinitembeza kila idara kunionyesha.

Muhingo akaendelea kuwa kaka yangu tuliyeheshimiana na kushirikiana. Kila nilipofika Habari Corporation akiwa Mhariri Mtendaji, Muhingo akioniona naongea na wanafamilia wengine chumba cha habari alikuwa akiniambia;

" Maggid, ukimaliza usiondoke bila kupanda juu ofisini kwangu tuongee."

Akiwa DC Handeni, nilikutana nae pale Chalinze kwenye mgahawa wa Kituo Cha Mafuta cha Kobil. Aliponiona alifurahi sana. Alinitambulisha kwa Mkurugenzi wake wa Halmshauri na kunikaribisha nifike Handeni nikaoene shughuli zinazofanyika huko na kushauri inapowezekana. Alinisisitiza. Bahati mbaya sikuweza kufika Handeni.

Akiwa DC Makete, Muhingo nilikutana nae kwenye Jengo la Akiba ( NSSF) Iringa.

Aliponiona alifurahi sana. Akanitamkia kama alichonitamkia Chalinze. Bahati mbaya tena sikuweza kufika Makete.

Kaka yangu Muhingo umeondoka nikiwa na mengi niliyojifunza kutoka kwako kupitia media. 

Nasikitika pia , sikuweza kukuona na kujifunza kutoka kwako kupitia Utumishi wa Umma kama kiongozi wa Serikali.

Kaka yangu Muhingo Rweyemamu, umeondoka nikiwa na hamu ya siku moja kukaa na wewe tukarejea mazungumzo yetu ya kwenye basi lile la Scandinavia kutoka Dar kwenda Iringa. Kufanya tathmini ya nini kimetokea na nini tafsiri yake.

Nitakukumbuka.

Maggid Mjengwa, 

Iringa.

Read 112 times

Add comment


Security code
Refresh

Tafuta Habari

Blog Shabihana

Simu