We have 153 guests and no members online

Mjawiri Awafunda Walimu Zanzibar

Posted On Monday, 09 October 2017 06:45 Written by
Rate this item
(0 votes)

Image result for Mmanga Mjengo Mjawiri

Na Khadija Khamis –Maelezo  Zanzibar

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali, imesema madai ya walimu juu ya maslahi mazuri, lazima yaende sambamba na utekelezaji wa majukumu yao ya ufundishaji kama inavyopasa.

Naibu Waziri wa wizara hiyo Mmanga Mjengo Mjawiri, amesema ufundishaji usiokidhi viwango ni miongoni mwa sababu kadhaa zinazoshusha kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi.

Akizungumza leo Oktoba 8, 2017 katika kongamano lililofanyika kwenye ukumbi wa Sanaa Rahaleo kwa ajili ya kuadhimisha ‘Siku ya Walimu Duniani, Mjawiri alisema walimu wengie hawayamudu masomo wanayofundisha.

“Ili mwalimu aweze kufahamika vizuri na wanafunzi wake, lazima kwanza alijue vyuema na alimudu somo lake ili fundishe kwa ufasaha na ustadi mkubwa,” alifahamisha.

Aidha, Naibu Waziri huyo alisema walimu wana wajibu wa kuzingatia misingi mikuu ya ufundishaji, mbinu na maadili ili kufikia malengo yanayotakiwa.

Alisema mbinu na uweledi unahitajika wakati wa kufundisha ili kuwawezesha wanafunzi wote, wale wenye uwezo mkubwa wa ufahamu na walio wazito, ili kuwafanya wanafahamu na kwenda sambamba na mwalimu.

Mjawiri alikumbusha kuwa, lengo la ‘Siku ya Walimu Duniani’, ni kuwatanabahisha umuhimu wa kujitathmini, kujifahamu na kujikosoa ili wafanikiwe katika jukumu la ulezi na ufundishaji walilokabidhiwa.

Aidha alieleza kuwa wizara yake imeweka utaratibu wa kutembelea skuli mbalimbali kwa lengo la kufahamu maendeleo ya wanafunzi pamoja na mpango mzima wa ufundishaji .

Alisema utaratibu huo utasaidia kufahamu viwango vya walimu katika kufundisha, na hivyo kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo na nyengine zinazokabili skuli hizo.

Hata hivyo, alisema tayari baadhi ya changamoto zimeanza kupatiwa ufumbuzi ikiwemo wingi wa wanafunzi unaosababisha msongamano na hivyo kuwafanya walimu kutosomesha kwa uhuru, utulivu na ufanisi.

Changamoto nyengine alizosema zimeanza kutatuliwa, ni malimbikizo ya posho za likizo  wanazodai walimu, vifaa vya kufundishia   na uhaba wa walimu.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Zanzibar (ZATU) Salim Ali Salim, alisema chama hicho kinapaswa kutumia fursa ya kipekee kutathmini utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa mwaka 1996 na Shirika la Kazi Duniani (ILO) pamoja na UNESCO, kuhusu hadhi ya kazi ya ualimu.

Walimu walioshiriki kongamano hilo wameishukuru Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kwa jitihada zake za kuhakikisha changamoto za kimaslahi, uhaba wa vifaa na mafunzo zinarekebishwa kadiri uwezo unavyopatikana.

Kaulimbiu ya mwaka huu katika maadhimisho ya Siku ya Walimu Dunaini, ni “Uhuru wa Ajira ya Walimu Humjenga Mwalimu.”

Read 60 times

Add comment


Security code
Refresh

Tafuta Habari

Blog Shabihana

Znateli