We have 141 guests and no members online

SERIKALI YAPIGA HATUA KUDHIBITI MAGONJWA YALIYOKUWA HAYAPEWI KIPAUMBELE

Posted On Thursday, 16 November 2017 05:29 Written by
Rate this item
(0 votes)

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto imefanikiwa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kwa asilimia 90 kupitia mpango wa kudhibiti magonjwa hayo hapa nchini NTD.

Hayo yamezungumzwa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Bakari Kambi wakati alipofungua semina ya uhamasishaji wa kupambana na magonjwa hayo kwa wahariri wa vyombo vya habari na Wakuu wa idara mbalimbali wa Wizara ya Afya jijini Dar es salaam.

“Tumepata mafanikio kwani mpaka kufikia Oktoba 2017 huu tumefanikiwa kupunguza ugonjwa wa matende na mabusha katika wilaya 95 sawa na asilimia 77 kati ya wilaya 120 na hivyo tumesitisha kutoa dawa katika wilaya hizo,” alisema Prof. Kambi.

Aidha Prof. Kambi amesema kuwa katika mafanikio hayo pia Serikali imefanikiwa kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa Vikope (Trakoma) katika wilaya 58 sawa na asilimia 82 kati ya wilaya 71 hapa nchini.

Kwa mujibu wa Prof. Kambi amesema kuwa kwa maeneo ya nyanda za juu hususani katika maeneo ya Rungwe, Kyela, ileje na Busekeleo wamefanikiwa kupima wananchi na kuonyesha kuwa maambukizi yamepungua na hivyo kuendelea katika wilaya zilizobaki.

Kwa upande wake Mratibu wa Kitaifa wa Mpango wa kupambana na Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Dkt. Upendo mwingira amesema kuwa wanajamii wanatakiwa wajitokeze katika kupata dawa za kujikinga na magonjwa hayo kwani muitikio ni mdogo na inaweza kusababisha madhara makubwa siku za usoni.

Aidha Dkt. Mwingira amesema kuwa Semina hiyo imelenga kuwaelimisha wahariri wa vyombo vya habari ili watoe kipaumbele katika kuhamasisha wananchi juu ya matumizi ya dawa za kukinga magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ambayo ni Matende na Mabusha, Usubi,Minyoo na Trakoma ili kuweza kutokomeza kabisa ugonjwa huo hapa nchini.

Na WAMJW-Dar es Salaam

Read 52 times

Add comment


Security code
Refresh

Tafuta Habari

Blog Shabihana

Znateli