We have 140 guests and no members online

MOI YAOKOA BILIONI TANO KWA KUPUNGUZA RUFAA ZA NJE YA NCHI

Posted On Tuesday, 21 November 2017 11:40 Written by
Rate this item
(0 votes)

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu (MOI) imeokoa zaidi ya shilingi Bilioni 5 ambazo zingetumika kusafirisha wagonjwa nje ya nchi kufuata matibabu baada ya MOI kuanzisha huduma za kibingwa ambazo awali zilikua hazipatikani hapa nchini.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii , Jinsia Wazee na watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya alipotembelea MOI na kukagua hali ya utoaji wa huduma, mazingira , miundombinu na kuwajulia hali wagonjwa pamoja na kukutana na menejimenti.

Akizungumza na menejimenti ya MOI, Dkt. Ulisubisya alipongeza kazi nzuri na kubwa inayofanywa ambayo imepelekea watanzania kupata huduma bora za kibingwa ambazo wangepaswa kuzifuata nje ya nchi.

“Mnafanya kazi nzuri sana, jambo ambalo linatupa faraja kubwa sisi viongozi wenu, naomba muongeze ubunifu zaidi, hamtakiwi kuifikiria MOI kwenye ukanda huu wa Afrika pekee bali duniani, hii ni changamoto kwetu sote kuifikisha hapo,” alisema Dkt. Ulisubisya

Aidha, Dkt Ulisubisya alisema MOI imepunguza rufaa za kwenda nje ya nchi kwa asilimia 95% na asilimia 5% iliyobaki MOI inaweza kuimaliza kabisa na kusiwepo mgonjwa wa kwenda nje ya nchi.

Pia, aliwaelekeza viongozi wa MOI kushirikiana na Wizara ya Afya kutafuta namna ya kufuta rufaa kwa kutoa mapendekezo na ushauri utakaosaidia kutatuliwa kwa changamoto hiyo.

“Azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt John Pombe Magufuli ni kuhakikisha huduma zote za Afya zinapatikana hapa nchini na vyema sote tukamuunga mkono,” alisema Dkt. Ulisubisya.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Muhamed Kambi alipongeza uongozi wa MOI kwa kuwa na maono ya mbali ya kuifanya MOI kuwa Taasisi bora barani Afrika na Duniani.

“Nimefurahi kwamba MOI mna maono ya mbali, mnafikiria kuitoa Taasisi hii hapa ilipo na kuifikisha sehemu ya juu zaidi, dira yenu ni kuwa Taasisi bora Afrika kufikia 2022 fanyeni kazi kwa bidii kufikia lengo hilo,” alisema Prof. Muhamad Kambi

Awali akiwasilisha taarifa ya Utendaji, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt Respicious Boniface alisema toka kuanzishwa kwa Taasisi hiyo imefanikiwa kuanzisha huduma za kibingwa za Upasuaji wa Nyonga, Magoti, Ubongo, Mgongo, Vibiongo, Usingizi ambazo zimesaidia kupunguza rufaa za nje ya nchi.

“Baada ya kuanzisha huduma hizi za Kibingwa tumefanikiwa kuokoa shilingi Bilioni tano ambazo zingetumika kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi, tumepunguza rufaa kwa asilimia kubwa naomba nikuhakikishie hata hizi asilimia 5% zilizobaki tutashirikiana na Serikali na naamini zitakwisha kabisa.” alisema Dkt. Respicious Boniface.

Na Patrick Mvungi – MOI

Read 36 times

Add comment


Security code
Refresh

Tafuta Habari

Blog Shabihana

Znateli