We have 133 guests and no members online

EU YAZINDUA MRADI WA KUPUNGUZA MIANYA YA RUSHWA NCHINI

Posted On Saturday, 25 November 2017 07:35 Written by
Rate this item
(0 votes)

Mradi unaolenga kupunguza mianya ya rushwa nchini unaofahamika kama “Tuungane Kutetea haki” umezinduliwa.

Akizungumza wakati akifungua mradi huo, jijini Dar es Salaam, Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) ambao ndio mfadhili wa mradi huo, Balozi Roeland Van der Geer, alisema mradi huu utasaidia kupunguza mianya ya rushwa nchini ambayo ni kikwazo cha maendeleo ya nchi.

Hata hivyo, Balozi Roeland Van der Geer alisema EU inaridhishwa na juhudi za Rais John Magufuli na serikali yake katika kupambana na rushwa, huku akisisitiza serikali kuzingatia uwazi katika uwajibikaji, ambapo amesema EU iko tayari kushirikiana na serikali katika vita hii.

“Rais Magufuli anafanya vizuri katika kupambana na rushwa, EU iko tayari kushirikiana na serikali yake kutokomeza Rushwa, Rushwa ni adui wa maendeleo na haiko Tanzania pekee, lakini ili kuitokomeza inabidi uwepo uwazi baina ya serikali na wananchi,” alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mradi wa “Tuungane Kutetea Haki”, Daniel El-Noshokaty alisema Tanzania inateseka kwa ugonjwa wa Rushwa na kwamba kufuatia hali hiyo EU imeamua kuanzisha mradi huu.

“Inabidi tuongeze jitihada za kupambana na rushwa, sababu rushwa inaathiri wananchi na maendeleo ya nchi kwa ujumla. Kwa pamoja tukishirikiana tutafikia lengo la kupunguza rushwa,” alisema.

Naye Meneja wa Mradi, Maria Kayombo alieleza kuwa, mradi huo lengo lake kuu ni kupunguza mianya ya rushwa na kukuza ushirikiano kati ya asasi za kiraia, wananchi na serikali za mitaa, kwa kupanua wigo wa siasa, kuongeza uwazi na uwajibikaji katika ngazi ya halmashauri.

“Mradi ulilenga kuwajengea uwezo wananchi katika kushiriki kwenye michakato ya maendeleo kama vile kuibua, kupanga, kutekelwza na kusimamia miradi ya maendeleo, pamoja na kuhakikisha serikali inatoa taarifa mbalimbali za maendeleo kwa umma kwa muda unaotakiwa, pia kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu, na miongozo ya serikali,” alisema.

Kayombo alisema mradi huo utafanyika katika kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka 2017 hadi 2019, utakaohusisha mikoa saba ikiwemo Geita, Simiyu, Ruvuma, Lindi, Mara na Kagera. Umegharimu Sh. 2.5 bilioni. Na umefadhiliwa na (EU) kwa kushirikiana na Taasisi ya Konrad Adenauer Stiftung (KAS) na Action For Democracy and Local Governance (ADLG) pamoja na asasi za kiraia 27 kutoka mikoa husika.

Na Regina Mkonde

Read 58 times

Add comment


Security code
Refresh

Tafuta Habari

Blog Shabihana

Znateli