We have 137 guests and no members online

SERIKALI KUANZA KUTUMIA MFUMO WA KIELETRONIKI KUTOA HATIMILIKI ZA VIWANJA

Posted On Wednesday, 29 November 2017 04:20 Written by
Rate this item
(0 votes)

Serikali itaanza kutoa hatimiliki za viwanja kati ya siku moja na siku saba kwa kutumia mfumo wa kielektroniki ifikapo Juni 1, 2018.

Hayo yameelezwa leo Novemba 27 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendelo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi wakati wa ziara ya kutembelea ofisi za Mfumo Unganishi wa Taarifa za Ardhi.

“Tunataka kupunguza urasimu na kuongeza ufanisi katika kutoa hati kutoka ilivyo sasa ambapo hati hutolewa kati ya mwezi mmoja hadi miezi mitatu,” alisema Lukuvi.

Ameongeza kuwa mfumo huo utaondoa udanganyifu katika kutoa hati kwa watu wawili au zaidi katika kiwanja kimoja na kuondoa migogoro ya viwanja ambayo imekuwa kero kwa wananchi.

Lukuvi amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuondoa utapeli uliokuwa ukifanyika kuhusu ardhi na ndio maana imeanzisha mfumo huo ambao ameuita muarobaini wa migogoro ya ardhi.

Aidha, Waziri Lukuvi alisema kuwa hati ya kisasa itakuwa na ukurasa mmoja badala ya zamani ambayo ilikuwa na kurasa zaidi ya ishirini.

Kwa mfumo huo, maafisa ardhi hawatatumia tena karatasi bali watakuwa na kompyuta ambamo taarifa zote zitahifadhiwa, aliongeza Lukuvi.

Lukuvi amesema kuwa mfumo utaiwezesha Serikali kuwafahamu wamiliki wote wa viwanja na kuwakumbusha muda wa kulipia viwanja vyao, hivyo mapato ya Serikali yataongezeka.

Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, Mfumo huo utatumika kutunza taarifa za ardhi za nchi nzima na hauwezi kuchezewa na mtu yeyote kwani kutakuwepo na nywila (password) ya kuingia kwenye mfumo ambayo itatolewa kwa maafisa wachache na hivyo kupunguza uwezekano wa kutoa hati zaidi ya moja kwa kiwanja kimoja.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na wataalam kutoka Kampuni ya IGN FI wanatekeleza, uundaji, usambazaji, usimikaji na uendeshajiwa mradi wa mfumo unganishi wa taarifa za ardhi unaodhaminiwa na Benki ya Dunia.

Dhumuni la mradi huo ni kuimarisha usalama katika umiliki wa ardhi kwa kuboresha usalama na usahihi katika manunuzi ya ardhi pamoja na kuanzisha mfumo sahihi na imara wa taarifa za ardhi.

Mfumo huo utakamilika ifikapo Juni 1 mwakani (2018) na hati ya kwanza ya kielektroniki ndipo itatolewa rasmi. Na wenye hati za zamani watatakiwa kubadilisha hati zao na kupewa za kielektroniki.

Na Jonas Kamaleki- MAELEZO

Read 51 times

Add comment


Security code
Refresh

Tafuta Habari

Blog Shabihana

Maji