We have 392 guests and no members online

WAZAZI WADAIWA KUWA CHANZO CHA UKATILI WA KIJINSIA KWA WATOTO WA KIKE

Posted On Thursday, 28 December 2017 04:03 Written by
Rate this item
(0 votes)

Imeelezwa kuwa vitendo vya ukatili wa kinjisia vimeendelea kufanyika mkoani Singida kwa kile kilichodaiwa ni wazazi wa pande mbili kumalizana kupitia mazungumzo pamoja na kunywa ‘supu’ ya mbuzi.

Hayo yamesemwa mkuu wa dawati la kijinsia mkaguzi wa Polisi, Iddah John, wakati akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku 16 kupinga ukatili wa kijinsia duniani yaliyofanyika kimkoa, katika kijiji cha Ilongero wilaya ya Singida.

Akifafanua, alisema mwanafunzi wa kike akipewa mimba, wazazi wa binti huyo humalizana kwa mazungumzo na wazazi wa mwanaume aliyesababisha mimba husika.

“Wazazi wa mwanafunzi huyo wa kike, huficha kwa makusudi  tukio hilo lisaijulikane kabisa.Wao watafanya mazungumzo na upande uliomfanyia binti ukatili wa kijinsia kwa kumbebesha mimba,i li hali ni mwanafunzi,” alisema na kuongeza.

“Kwa ujumla kwenye mazungumzo hayo, yatafanyika makubaliano ya upande ulioathirika kupata ‘kitu kidogo’, na kisha kitakachofuata ni  kunywa ‘supu’ ya mbuzi”.

Akifafanua zaidi,Iddah alisema ni ukweli usiopingika kwamba wazazi hao, watakuwa wamemfanyia ukatili wa kijinsia binti yao, kwa vile atakuwa amekatishwa kuendelea na masomo yake.

Mratibu huyo, alitumia fursa hiyo kuihimiza jamii mkoani hapa kutoa ushirikiano katika  kusaidia kutokomeza vitendo hivyo, pamoja na ukeketaji. Wasaidie kwa kutoa taarifa sahihi zinazohusu vitendo hivyo, ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua stahiki.

Kwa upande wake, mgeni rasmi katika maadhimisho hayo yaliyofana, kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Singida, Veronica Mure, alisema ukatili wa kijinsia unafanywa na kila mtu, kwa kujua na kwa kutokujua.

“Kwa hali hiyo, vitendo hivi ambavyo vipo kinyume na haki za binadamu,ni jukumu letu sisi sote kuvitokomeza. Tunapaswa tujitambue na tuamue kwa dhati kushiriki kuvitokomeza vitendo hivi. Serikali, asasi na mashirika yasiyo ya kiserikali, yasaidie tu mapambano haya, lakini sisi sote tuwe mstari wa mbele,” alisema Mure.

Akisisitiza, kaimu mkurugenzi huyo,alisema jamii ina mapungufu katika mapambano haya, ikiwemo kushindwa kutoa ushirikiano na vyombo vya sheria katika kuvitokomeza.

“Kitendo cha ukatili wa kijinsia au ukeketaji, kikitolewa taarifa polisi au mahakamani, kwanza mhanga wa tukio atafichwa, na mbaya zaidi, hakuna mtu watakaokuwa tayari kushirikiana na polisi au kutoa ushahidi mahakamani. Tabia hii inachangia sheria kusindwa kuchukua mkondo wake,”alisema.

Wakati huo huo,mratibu wa shirika lisolo la kiserikali la MEDO Action Aid Tanzania, wilaya ya Sigida, Agness  Akwilini, ametumia nafasi hiyo kuwasihi wakazi mkoani hapa, kufunguka na kutoa taarifa za vitendo vya ukatili wa kijinsia na ukeketaji kwa mamlaka zinazohusika.

Amedai kwamba  visipo fichuliwa, hakuna mtu atabaki salama bila kuathirika moja kwa moja au kwa njia nyingine.

“Serikali imejitahidi sana na imefanya jambo jema la kuajiri maafisa maendeleo ya jamii hadi ngazi ya kata. Tuwatumie vizuri maafisa hawa kwa kuwapatia taarifa sahihi za vitendo vya ukatili wa kijinsia na ukeketaji. Tukiwatumia vizuri maafisa hawa, tutatokomeza kabisa vitendo hivi ambavyo havikubaliki,” alisema Agness.

Na Nathaniel  Limu, Singida

Read 29 times

Add comment


Security code
Refresh

Tafuta Habari

Blog Shabihana

Smart