We have 221 guests and no members online

WAZIRI MKUU AWASILISHA TAMKO LA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA

Posted On Saturday, 30 December 2017 15:05 Written by
Rate this item
(0 votes)

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema amekwishawasilisha tamko la viongozi wa umma kuhusu rasilmali na madeni kwenye Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma tangu jana (Alhamisi Desemba 28, 2017).

Akizungumza na waandishi wa habari kijijini kwake Namahema ‘A’ wilayani Ruangwa mkoani Lindi, Waziri Mkuu amesema fomu hizo zilipokelewa jana na amekwishapatiwa barua ya kupokea tamko hilo.

“Nimewaita hapa ili kuthibitisha kuwa nimetekeleza takwa hilo la kisheria na tayari Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi ya Umma imekiri kupokea tamko langu kwa barua hii hapa,” alisema Waziri Mkuu huku akionyesha barua hiyo ambayo ilisainiwa na Kamishna wa Maadili, Jaji (mst.) Harold Nsekela, Desemba 28, 2017,

“Kwa kuzingatia mfano ulioonyeshwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, ninawaagiza viongozi wote wanaotakiwa kujaza fomu hizo kwa mujibu wa sheria, wafanye hivyo na kuziwasilisha ifikapo tarehe 31 Desemba, 2017 saa 10 jioni,” alisisitiza Waziri Mkuu.

Alisema anawakumbusha Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu wote na viongozi wote walioko kwenye ngazi za uteuzi wahakikishe wanatimiza takwa ambalo liko kwa mujibu wa kifungu cha 9 na cha 11 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya Mwaka 1995.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwatakia Watanzania wote heri wakati wanaposubiri kumaliza mwaka 2017 na kuwatakia heri na fanaka katika maeneo waliyopo wanapojiandaa kuupokea mwaka 2018

Read 42 times

Add comment


Security code
Refresh

Tafuta Habari

Blog Shabihana

Znateli