We have 185 guests and no members online

Tambaza, Miaka 34 Iliyopita!

Posted On Sunday, 14 January 2018 09:18 Written by
Rate this item
(0 votes)

 

Ndugu zangu,

Asubuhi ya Jumatatu ile ya tarehe 14 mwezi Januari mwaka 1984 tulikusanyika kuanza Form One pale Tambaza Boys Sekondary School, Upanga, Dar es Salaam.

Haraka sana niliiona familia mpya; Tambaza Family. Wana-Tambaza tuliishi kama ndugu.

Kama wanafunzi, hatukupenda kuonewa, kuonea, na wala kuwaona wanafunzi wa shule nyingine wakionewa .

Kuna mengi niliyojifunza nikiwa Tambaza, kinadharia na vitendo. Naikumbuka Jumamosi moja tukiwa Kidato Cha Pili, mmoja wa walimu wangu, marehemu Mwalimu D. J. Mkomagu aliniachia somo maridhawa. Mwalimu Mkomagu alishiriki kutunga kitabu cha riwaya ya ' Zaka la Damu' akiwa na Harrison Mwakyembe kama kazi ya kitaaluma wakiwa shuleni. Kitabu hicho kikaja kutumika mashuleni.

Ilikuwaje basi Jumamosi ile;

Ni hivi, kuna vyoo vya shule viliziba. Havikutumika kwa muda mrefu. Siku hiyo Mwalimu Mkomagu alitutaka wote tufike shuleni tukiwa na nguo za kazi. Naye alivalia jeans na buti kubwa.

Alitamka;

" Hatuwezi kusubiri Wizara ya Elimu ije kutuzibulia vyoo vyetu. Kazi hiyo tutaifanya wenyewe."

 

Leo tungemwita Mwalimu Mkomagu ' Mzee wa Hapa Kazi Tu'.

Kama utani, Mwalimu Mkomagu aliongoza operesheni ile kwa vitendo. Tulikuwa naye katika kila hatua. Na hakika, ndani ya saa nne, vyoo vile vikazibuliwa na kuanza kutumika.

Kikubwa nilichojifunza kutoka kwa Mwalimu Mkomagu ni kuwa Uongozi si kusimamia tu, bali ni kushiriki kwa vitendo katika kukifanya kile, kama kiongozi, umewataka wengine wafanye.

Nilichokikosa Tambaza? Wasichana.

Ilikuwa ni shule ya wavulana watupu. Naamini, kuwa kwa miaka minne nilikosa mitazamo ya wasichana katika masuala mbalimbali tuliyokuwa tukisoma na kuyajadili. Bila shaka, ingenisaidia mimi na wengine wengi katika kupanua uelewa wa masuala mbali mbali.

Naam, ni wakati wa kutafakari na kujiuliza pia, kuwa hata katika wakati huo, tulikuwa na ndoto gani kwa nchi yetu.

PS: Pichani kutoka kushoto; Shaban Nduku, mimi, Mussa Twaha Kitonge na Ngaja Mussa Mchele.)

Maggid.

Read 39 times

Add comment


Security code
Refresh

Tafuta Habari

Blog Shabihana

Watumishi