We have 136 guests and no members online

Filamu Ya ' The Post' Imenikumbusha Mohammed Ali..

Posted On Sunday, 21 January 2018 12:26 Written by
Rate this item
(0 votes)

Image may contain: 4 people, people standing

Image may contain: 2 people, people sitting, table and indoor

 

Ndugu zangu,

Jana mke wangu mpenzi na mimi tulikwenda kuangalia filamu ya The Post. 
Ni mara chache sana mwisho wa filamu unatamani kushangilia kama uko uwanjani kwenye mpira.

Filamu iliyoanza taratibu ilipamba moto katikati na kumalizika kwa kishindo.

Inahusu Vita ya Vietnam na sakata la nyaraka za siri za Pentagon ambazo mwandishi wa The Washington Post alizifanyia kazi. Pamoja na vitisho vya White House, gazeti la Washington Post hatimaye liliweka hadharani ukweli mzima kwa watu wa Marekani.

Pentagon, Idara ya Ulinzi ya Marekani wakati vita vikiendelea ilificha ukweli wa jinsi Marekani ilivyokuwa ikishindwa vita hivyo.

Filamu pia inampa nafasi Mwanamke. Ni pale mwanamama Meryl Streep alivyocheza kwa umahiri mkubwa nafasi ya kuwa mmiliki wa gazeti. Akahimili vitisho na akatoa kauli ya mwisho ya gazeti kuchapwa.

Filamu hii inanikumbusha kisa nilichowahi kuandika hapa juu ya Muhammed Ali na vita vile vya Vietnam mara ile ulimwengu ulipofikiwa na habari za kifo chake. Niliandika..

"Muhammed Ali, Daima Alikataa Kuwa Mbeba Mabuli..

Ndugu zangu,

Usiku wa kuamkia leo ulimwengu umefikiwa na habari za kifo cha mwanamasumbwi mahiri kupata kutokea hapa duniani, ni Muhammad Ali.

Muhammad Ali, atakumbukwa kama shujaa wa wanyonge wa dunia. Alikuwa bondia na mwanaharakati wa haki za wanyonge. Daima Ali hakukubali kuburuzwa.

Hapa nyumbani, Rais Mstaafu , Mzee Ali Hassan Mwinyi amejaliwa kipawa cha kutumia vema lugha ya Kiswahili anapowasilisha ujumbe wake. Kuna wakati alipata kutamka;

“ Ndugu zanguni, kuna wasafiri na wabeba mabuli!”.

Wabeba mabuli ni wale wanaotumiwa safarini kwa kazi ya kubeba hiki na kile, ni kama wapagazi. Wabeba mabuli ni watu wa kuamrishwa safari bila kujua inakwenda wapi. Lakini wabeba mabuli anaowazungumzia Mzee Ali Hassan Mwinyi ni viumbe wenye kufikiri.

Bondia Mohammed Ali alipata kuvuliwa ubingwa wa uzito wa juu duniani kwa kukataa kwenda kupigana vita Vietnam. Alipotakiwa aende vitani Mohammed Ali alikataa na kusema;

“ Siwezi kwenda Vietnam kwa vile sijui hao tunaokwenda kuwapiga wana kosa gani”

Mohammed Ali akaambiwa , kuwa wenzake wameshakwenda huko Vietnam, naye akajibu; 
“ Hao waliokwenda huenda wameshaambiwa kosa walilofanya Wa- Vietnam, miye bado sijalijua”.

Naam. Mohammed Ali hakwenda Vietnam, ni kiumbe aliyefikiri na aliyekataa kuwa mbeba mabuli. Waliompa Mohammed Ali adhabu ya kunyang’anywa mkanda wake wa ubingwa na hata kufungiwa kucheza ngumi kwa muda fulani bado wanamuheshimu Mohammed Ali kwa msimamo wake ule.

Muhammad Ali atakumbukwa daima."

PS: Picha ya juu ni siku Mohammed Ali apotua Dar es Salaam.

Maggid.

Read 44 times

Add comment


Security code
Refresh

Tafuta Habari

Blog Shabihana

Smart