simulizi

Kumbukumbu: Miaka 12 Baada Ya Kifo Cha Nguli Tx Moshi William.

on

Sauti yake ilikuwa ya kuvutia, alitunga nyimbo zenye hisia kali nyingi za tungo zake zilitokana na maswahibu ya maisha yake. Jina lake hasa ni Shaaban Mhoja Kishiwa ingawa amekuwa akijulikana zaidi kwa jina la Moshi William TX, aliyezaliwa mwaka 1958 katika wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.

Wanamuziki wa Bendi ya Msondo ngoma wamesema kuwa pengo aliloliacha Mwanamuziki mwenzao TX Moshi William halitazibika kamwe.

Mwanamuziki huyu maarufu Tanzania na sehemu mbalimbali hasa Afrika Mashariki na ya kati aliaga dunia March 29, 2006 na kuzikwa siku hiyo hiyo katika makaburi ya Keko machungwa jijini Dar es salaam.

Aliacha mke na watoto watano, wawili wa kike na watatu wa kiume. Mwanamuziki huyo aliaga dunia siku ya Jumatano asubuhi majira ya saa tatu. Kwa mujibu wa Mke wa mwanamuziki huyo, Bi Asha Seif, William alikufa kutokana na tatizo la mguu pamoja na figo.

Mguu huo ulivunjika katika ajali ya gari aliyoipata Desemba 16, mwaka 2005, na mwezi Februari 13, mwaka 2006 akalazwa Hospitali ya Burere Kibaha. Baadae ilibainika kuwa mguu huo ulianza kumsumbua na kutunga usaha kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Regency Machi 15 baada ya kugundulika kwamba alikuwa na  matatizo ya figo. Machi 18, alihamishiwa Muhimbili kwenye kitengo cha kushughulikia mifupa MOI.

TX alijiunga na Kundi hilo mwaka 1982 akitokea Polisi Jazz na miongoni mwa nyimbo alizotunga mara baada ya kujiunga na bendi hiyo ni pamoja na Ajuza, Asha Mwanaseif, (aliomtungia mkewe), na wimbo mwingine Ashibaye.

Muimbaji huyo alitunga nyimbo nyingi baada ya kuhamia kwenye bendi hiyo lakini nyimbo zilizotia fora sana ni pamoja na Kilio cha Mtu Mzima, Ndoa Ndoana, Piga Ua Talaka Utatoa, Isihaka Kibene, Kaza Moyo, Harusi ya Kibene, na Ajali.

Wimbo wa Ajali aliutunga mara baada ya kupata ajali iliyompelekea kuvunjika mguu. Na ni mguu huo huo unaosemekana kusababisha mauti yake pamoja na ugonjwa wa figo.

Bendi hii ya Msondo Muziki ilizaliwa kutoka Bandi ya OTTU ambayo pamoja na kubadilishwa jina mara kwa mara ilianzishwa mwaka 1964, ikiwa sehemu ya tawi la Chama cha wafanyakazi nchini National Workers Union. Wakati huo ilipoanzishwa ilikuwa ikiitwa NUTA. Baadae jina hili likaja kubadilishwa na kuitwa Juwata Jazz Band mnamo mwaka 1977, na kisha kuitwa OTTU.

Mwanamuzi Said Mabera aliyefanya kazi kwa karibu na TX aliwahi kusema kuwa kama kuna kitu ambacho kilimpa sana heshima kubwa mwanamuziki huyu William ni uwezo wake wa kutunga na kuimba, tofauti na wanamuziki walio wengi ambao unaweza kukuta mwanamuziki anajua kuimba lakini hana uwezo wa kutunga nyimbo au ana uwezo wakutunga lakini hana sauti nzuri.

Safari yake kimuziki, Bwana Moshi mwenyewe wakati wa uhai wake aliwahi kusema kuwa amepitia katika bendi mbalimbali za muziki ambazo ni pamoja na Safari Trippers, Juwata Jazz. UDA Jazz, na Polisi Jazz, ambayo alitokea wakati anajiunga na kundi hili.

Wakati wa uhai wake pia alijaliwa kupata tuzo mbalimbali za muziki hasa zile zijulikanazo kama Kilimanjaro Music Award.

Baadhi ya vyombo vya habari nchini Tanzania vilikariri kuwa Moshi alibatizwa jina la TX, na Mwandishi wa Habari wa siku nyingi aliyekuwa mtangazaji wa Radio Tanzania, Julius Nyaisanga kwamba Nyaisanga alimbatiza jina hilo kutokana na tunzi zake za uhakika.

Mengi hayafahamiki kwenye maisha yake inagawa wakati Fulani alikaririwa akisema kuwa hali hii ya kutotulia sehemu moja hasa wakati akiwa mtoto ilitokana na ugomvi baina ya Mama yake na Baba yake.

Kwa hakika Moshi William aliacha pengo kubwa ambalo halitazibika katika ulimwengu wa muziki wa Dansi Tanzania, kama alivyothibitisha Bwana Waziri Dewa ambaye ni mratibu wa shughuli za Bandi hiyo ya Msondo, kwamba itakuwa kazi ngumu na isiyofikiriwa kumpata mwimbaji mwingine mwenye sauti yenye mvuto kama ya TX Moshi William.

R.I.P TX  MOSHI WILLIAM.

About Muhammed Khamis

hosearevocatus9@gmail.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *