habari

Lugola Awataka Majambazi Wajisalimishe Pamoja Na Silaha Zao.

on

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewataka majambazi popote walipo nchini kujisalimisha pamoja na silaha zao wakati Polisi wakiendelea na msako mkali mpaka jambazi wa mwisho anatiwa mbaroni. Lugola amesema Jeshi la Polisi lipo imara na litawasaka majambazi hao usiku na mchana popote walipo na litahakikisha nchi inaendelea kuwa salama na wananchi wema wakiendelea kufanya shughuli zao za maendeleo kwa kulijenga Taifa.

Akizungumza na mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Kasahunga, Kata ya Neluma, Jimbo la Mwibara, Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, leo, Lugola amesema usalama wa nchi hauchezewi na mtu yeyote na watu wasijaribu kutikisa kiberiti kwa kulichezea Jeshi la Polisi. Lugola amesititiza kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano ambayo inaongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli, ujambazi hauna nafasi na pia amewataka majambazi hao wafanye kazi nyingine ya kuwaingizia kipato kwa njia halali.

“Msijaribu kukitikisa kiberiti, Serikali ipo macho muda wote, Jeshi lenu lipo imara, majambazi wanaofanya uvamizi, tutahakikisha tunawasaka popote walipo jambazi mmoja baada ya mwingine, hatutalala wala kupumzika hadi jeshi letu litakapomtia mbaroni jambazi wa mwisho,” alisema Lugola.
Kutokana na msako huo, Lugola alisema majambazi hao wajisalimishe wenyewe pamoja na dhana zao kwenye kituo cha polisi wanachoona kipo jirani na wao, vinginevyo hawatasalimika na hawatabaki salama.

“Kama kuna ndugu zetu, watoto wetu, majirani zetu tuwaambie serikali hii ya magufuli nafasi hiyo ya kufanya ujambazi haipo, nimepata taarifa za uhalifu, wizi wa mifugo na uvamizi wa aina mbalimbali, tuone taarifa polisi ili tuweze kuwatia mbaroni majambazi hao kwa wale wote ambao mnahisi wanajihusisha na uhalifu, toeni ushirikiano bila woga ili meneo yetu yazidi kuwa na amani,” alisema Lugola.

Hata hivyo, Lugola alisema ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo ndani ya Wizara yake ambavyo anavisimamia wapo baadhi ya askari wachache ambao wanajihusiha na vitendo vya rushwa na alishatoa onyo mara nyingi, hivyo atakao wakamata hatawaonea huruma. “Kuna baadhi ya mazingira ambayo yanachangia rushwa zaidi ndani ya Jeshi la Polisi ikiwemo kutokutolewa kwa dhamana katika siku za mapumziko Jumamosi na Jumapili, baada ya kuona kunamianya ya rushwa nikatangaza nchi nzima vituo vyote vya polisi vitoe dhamana saa 24 na siku 365 na robo, pia kutowekwa mahabusu watuhumiwa ambao wanamakosa madogo madogo,” alisema Lugola.

Lugola anaendelea na ziara jimboni kwake ya kuhamasisha wananchi kuanza maandalizi ya kilimo pamoja na kuendeleza miradi ya maendeleo huku wakiendelea kuheshimu sheria za nchi.

About Muhammed Khamis

hosearevocatus9@gmail.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *