habari

Maonesho ya NaneNane Kitaifa Kufanyika Mkoani Simiyu Kwa Miaka Mitatu Mfululizo

on

Na Mathias Canal, WK-Simiyu
Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba ametangaza kuwa maadhimisho ya maonesho ya kilimo na sherehe za wakulima Nanenane Kitaifa yatafanyika Mkoani Simiyu kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2018 mpaka 2020 ili kuongeza tija ya elimu kuhusu sekta ya kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa wananchi wa kanda ya Ziwa Mashariki.
Waziri wa kilimo Mhe Tizeba ametanga neema hiyo kwa wananchi wa kanda ya ziwa Mashariki jana tarehe 8 Agosti 2018 kwa wakazi wa mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara ambayo inaunda kanda ya ziwa Mashariki ambao watanufaika na elimu kuhusu kilimo, mifugo na uvuvi.
Alisema kuwa kumekuwa na utaratibu wa kufanyika mfululizo maonesho hayo kwenuye mikoa inayoandaa huku akieleza kuwa utashi uliopo katika kanda hiyo ni mkubwa ukilinganisha na maonesho ya Nanenane yaliyofanyika kwa miaka minne mfululizo katika Viwanja vya Ngongo Mkoani Lindi.
Alisema kuwa kufanyika mfululizo kwa miaka mitatu mkoani Simiyu kutawafanya wananchi kuwa na uhakika wa bidhaa za uwekezaji watakazoziweka. “Mkoa wa Simiyu na kanda yenu hii ya Magharibi ingetosha kuonyesha hata kwa miaka miwili tu lakini nimeamua kutumia utaratibu mzuri zaidi ili ifanyike kwa miaka mitatu naamini hamtaniangusha” Alikaririwa Mhe Dkt Tizeba
Aliwataka wakuu wa mikoa ya Shinyanga Mhe Zainab Telack, Mkoa wa Mara Mhe Adam Malima na Mkoa wa Simiyu Mhe Antony Mtaka kuyafanya maonesho ya Nyakabindi katika miaka miwili ijayo kuifanya sherehe hiyo ya Nanenane kuwa ya kimataifa ili kuwe na washiriki kutoka katika nchi zote nane zinazoizunguka Tanzania.
Alisema kuwa ingependeza zaidi kuwa na washiriki wa maonesho ya teknolojia na mambo mbalimbali ya kilimo kutoka katika nchi hizo za jirani ili kubadilishana uzoefu katika kuinua sekta ya kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Waziri Tizeba alisema kuwa nchi ya Tanzania ndiyo kinara katikja kilimo katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati hivyo maonesho ya kilimo yanapaswa kuwa katika mpango madhubuti wa kufikia maonesho ya kimataifa.
“Naomba niwaahidi hapa kuwa sisi kama wizara tutatoa ushirikiano mzuri ili kuhakikisha kuwa maonesho yajayo yanakuwa katika sura ya kimataifa kwani kufanya hivyo tutakuwa tumeongeza ufanisi na elimu pana kwa wakulima wetu  wa chini” Alisisitiza Mhe Dkt Tizeba
Sambamba na hayo pia Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba alimshukuru Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Benjamin Mkapa kwa kukubali kuwa mgeni reasmi katika kilele cha maonesho ya Nanenane Kitaifa kwani amekuwa chachu na hamasa katika kuongeza ufanisi na tija kwenye sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Dkt Tizeba alieleza kuwa kanda hiyo ya Ziwa Magharibi ya Nanenane ilianzishwa kwa wazo la Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Antony Mtaka ambaye alitaka kutoa fursa ya urahisi wa hudua ya mafunzo kwa wananchi kufahamu mbinu mbalimbali za kilimo, Ufugaji na Uvuvi.

About Muhammed Khamis

hosearevocatus9@gmail.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *