michezo

Monchi Atafanya Makubwa FC Roma

on

Na Olle Bergdahl Mjengwa

MSOMAJI, Sevilla ni timu ambayo katika miaka ya hivi karibuni imepata mafanikio makubwa sana. Walishinda Ligi ya Ulaya maarufu kama Europa League mara tatu mfululizo katika misimu ya 2013/2014—2014/2015 na 2015/2016. Hakika,  Sevilla wamekuwa na makocha wazuri kama Unai Emery na Jorge Sampaoli ambao wamekuwa sababu kubwa ya mafanikio ya Sevilla.

Lakini sababu nyingine ya Sevilla kufanya vizuri katika miaka ya hivi karibuni ni mwenyekiti wao wa usajili wa zamani Monchi. Tangu Monchi alipopewa cheo cha mwenyekiti wa usajili katika klabu ya Sevilla mwaka 2000 timu hiyo iliweza kusajili wachezaji wengi wenye kiwango kikubwa kwa bei nafuu na kuwauza kwa bei kubwa.

Ni wachezaji kama Dani Alves, Adriano, Ivan Rakitic, Alvaro Negredo na Seydou Keita. Bila shaka,  Monchi ana jicho zuri la kusajili wachezaji wenye vipaji vikubwa na ndio maana washabiki wa AS Roma walifurahi sana Monchi alipotangaza kwamba atakuwa mwenyekiti mpya wa usajili wa timu hiyo mwezi wa nne mwaka jana.

Roma ni klabu ambayo katika misimu ya hivi karibuni imeanza kuwapa Juventus upinzani katika Ligi Kuu ya Italia lakini kabla msimu huu walihitaji kusajili wachezaji wapya katika safu ya katikati na safu ya ushambuliaji kama kweli watakuwa na uwezo wa kushinda Ligi Kuu ya Italia.

Washabiki wengi wa Roma wamekuwa na matarajio makubwa kwamba Monchi ataweza kusajili wachezaji wazuri na kuifanya timu ya Roma kuwa imara zaidi. Lakini, katika dirisha kubwa la uhamisho mwaka jana Roma pamoja na Monchi waliamua kumuuza winga wa timu hiyo Mohamed Salah kwa klabu ya Liverpool. Hivi sasa inaonekana kwamba uamuzi wa Monchi haikuwa sahihi kwa kuwa Salah ameendelea zaidi kimpira msimu huu na amekuwa kati ya wachezaji bora zaidi barani Ulaya.

Hata hivyo ni muhimu kukumbuka kwamba ilikuwa lazima kwa Monchi kumuza mchezaji kama Salah kutokana na madeni makubwa ya Roma na mshahara mkubwa wa mchezaji huyu.

Wiki hii Roma wanacheza mchezo wao wa pili dhidi ya Liverpool katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa. Licha ya kufungwa magoli matano kwa mbili katika mechi ya kwanza dhidi ya Liverpool bado naamini kwamba timu hiyo huenda italipiza kisasi na kuwafunga Liverpool.

Na hata kama Roma wanatolewa katika Ligi ya Mabingwa basi lazima tumpongeze Monchi kwa kuwa ameweza kuisaidia Roma kujenga kikosi kizuri sana hata kama alimuuza mchezaji wao bora. Katika dirisha kubwa la uhamisho mwaka jana Monchi hakuwa na bajeti kubwa ya kusajili wachezaji. Lakini, aliweza kusajili wachezaji wenye bei nafuu na kiwango kikubwa kama Schick, Fazio na Juan Jesus ambao wote wamekuwa wachezaji muhimu sana katika mafanikio ya Roma katika Ligi ya Mabingwa msimu huu.

 Baada ya msimu huu naamini kwamba Monchi atapata bajeti na fedha nyingi zaidi kusajili wachezaji katika dirisha kubwa la uhamisho. Na Roma bado wanasaka mchezaji mwenye uwezo wa kurithi nafasi ya Francessco Totti katika kikosi hicho.

Sidhani kwamba kuna mchezaji mwenye uwezo wa kuvaa viatu vya Totti Roma. Lakini, kama yupo basi Monchi atamtambua.

Inawezekana

-Mwisho-

About Innocent Chambi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *