habari

Naibu Waziri Elimu Z’bar aahidi kushirikiana na Pennyroral

on

Na  Moh’d Haji ,Zanzibar

Naibu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Simai Mohamed Said amesema Serikali ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na taasisi ya Pennyroral katika jitihada za kuimarisha sekta ya elimu nchini ambayo ni nguzo muhimu ya kufikia maendeleo ya kweli.

Naibu Waziri huyo alibainisha hayo katika hafla ya kuwazawadia wanafunzi wa shule za Kijini na Mbuyutende katika kijiji cha Matemwe wilaya ya Kaskazini ‘A’, waliofanya vizuri kwenye masomo ya Kingereza na Hisabati mwaka 2018, chini ya ufadhiliwa wa taasisi ya ‘Best of Zanzibar’ .

Katika ghafla hiyo wanafunzi 50 waliofanya vizuri katika masomo ya Hisabati na Kingereza walikabidhiwa zawadi maalum ikiwamo vifaa vya masomo shuleni, ikiwamo ni hatua ya kuongezea ari wanafunzi weengine wa shule hizo kupenda kusoma masomo hayo..

Naibu Waziri, Simai alisema serikali inathamini mchango unaotolewa na taasisi binafsi na nchi washirika wa maendeleo katika kuwajengea mazingira mazuri wanafunzi wa Zanzibar ili kuinua kiwango cha elimu.

Naibu Waziri huyo alikishukuru kitengo cha ‘Best of Zanzibar’ kwa kubuni mradi huo kwa lengo la kuwakomboa wananchi wa Mkoa huo ambao kwa muda mrefu wamekuwa nyuma katika elimu hasa kwa masomo ya Kingereza na Hisabati.

Naibu Waziri huyo alifahamisha kuwa, mafanikio yaliyopatikana kwa wanafunzi hao katika masomo ya kingereza na hisabati, ni matunda ya jitihada za walimu wa skuli zote mbili pamoja na mchango wa Pennyroyal Ltd kupitia kitengo chao cha huduma za jamii, ‘Best of Zanzibar.’

Aidha aliwashukuru wanajamii nzima wakiwemo wazazi na walimu kwa  kuonyesha ushirikiano wao mkubwa kwa waendeshaji wa mradi huo, huku akiwataka kuzidi kuwahimiza vijana wao kuzidisha bidii kwenye masomo yao ili wafanikiwe katika maisha yao.

Naye Mratibu wa Elimu na Uwezeshaji wa ‘Best of Zanzibar’ Ali Hamad Suleiman mafanikio ya wanafunzi hao kufanya vizuri katika masomo ya Hisabati na Kingereza yametokana na uwepo wa walimu wa masomo hayo katika shule hiyo ambao wanasimamiwa na taasisi yao.

“Baada ya kubaini kuwa shule Matemwe kuwa nyuma kielimu hasa katika masomo ya Hisabati na Kingereza, kupitia mradi wetu huu tumeajiri walimu sita wa masomo hayo ambao tunawalipa sisi, ila walimu hao kazi yao ni kuwafundisha wanafunzi wa shule hizo tu, leo hii naona tumefarajika Sanaa kuona mabadiliko hayo”alisema.

Hamad alisema kutokana na mafanikio hayo wameona ni vyema kuongeza walimu wengine sita wa masomo ya sayansi ambao watafanya kazi kwa kushirikiana na walimu wakuu katika kufundisha masomo ya Fizikia, Kemia na Biolojia ili kuwawezesha wanafunzi kujiandaa na mabadiliko ya ulimwengu.

“Katika kuzidi kuwapa hamasa wanafunzi hao, tumewatangazia, ufadhili wa kwenda kusoma masomo ya Enginer kwa wale watakaofanya vizuri katika masomo ya sayansi katika mitihani yao ya taifa”alisema.

Naye Mkurugenzi Idara Maandalizi, Msingi na Kati, Safia Ali Rijali alisifu jitihada za taasisi hiyo katika kuunga mkono jitihada za serikali katika sekta ya elimu, huku akiwaasa wanafunzi, wazazi na walezi kuitumia vyema fursa hiyo ili kuleta mabadiliko ya kielimu katika Kijiji hicho.

Kwa upande wa  Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo iliyomo ndani ya Kampuni ya Pennyroyal Ltd, Brian Thompson aliwataka wanafunzi kusoma kwa bidii ili waweze kufikia matarajio yao na kuleta mabadiliko chanya katika jamii yao na taifa kwa jumla.

Alisema kampuni yao kupitia taasisi hiyo haitasita kuendeleza kutoa misaada ya kielimu katika kijiji hicho, jambo kuwa ni kuhakikisha kwamba misaada inayotolewa yende sambamba na mabadiliko ya kielimu.

Baadhi ya wanafunzi na wazazi walioshiriki katika ghafla hiyo wameahidi kutoa kila ya aina ya ushirikiano wao kwa taasisi hiyo juu ya kukuza elimu katika kijiji chao.

Jumla ya wanafunzi 632 wa shule hizo wananufaika na mradi huo unaoendeshwa chini ya ufadhili wa kampuni ya Pennyroyal Ltd, ambapo miongoni mwa mambo mengine, pia unakwenda sambamba na kampeni ya ‘Valisha mtoto viatu ambapo wanafunzi 400 walivishwa viatu’.

About Muhammed Khamis

hosearevocatus9@gmail.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *