simulizi

Neno La Leo: Kuishi Jirani Na Mahakama Si Kujua Sheria..

on

Ndugu zangu,

Fikiri kama Socrates angekuwepo kwenye mkusanyiko huu! Naam, mwenye hekima ni yule anayetambua kuwa hajui. Pichani ni tukio la ajali ya magari mawili kukwaruzana kwenye makutano ya Mtaa Livingstone na Mkunguni eneo la Kariakoo.

Ajali hii nilipata kuishuhudia kwa macho yangu, maana, nilisimama kando ya eneo hilo nikinywa maji ya madafu.

Kwanza, madereva walishuka na kuanza kulaumiana. Kila mmoja alimwona mwenziye ndiye mwenye kosa.

Wakafika wapita njia wengine wawili. Na ndani ya dakika tatu, kundi kubwa likakusanyika mahali hapo.

Hapo kukawepo na wajuaji wa sheria za barabarani. Wengine wakajitokeza kuwa mahakimu wa shauri, na mashahidi pia wakapatikana, hata wale ambao hawakuwepo kabisa wakati tukio likitokea.

Inatukumbusha mwanafalsafa Socrates wa Uyunani ya Kale. Socrates alipokuwa akichipukia kama mwanafalsafa katika mji wa Athens, alikumbana na upinzani mkubwa. Maana, Athens ilikuwa na Masophisti walioaminika kuwa walijua mengi.

Ndio hao waliotafsiri mambo ikiwamo sheria pia. Ndio hao waliodhaniwa kuwa ni wajuzi wa kutunga mashairi .

Ndio walioaminika kuwa waliujua ukweli. Lakini, kwa masophisti, ukweli ulikuwa ni relative. Kwao wao, ukweli ulikuwa ni ukweli kama ukweli una maslahi kwao.

Hivyo basi, jambo ambalo lilisemwa kuwa ni ukweli leo, kesho laweza kuwa ni uongo kulingana na mazingira ya wakati huo.

Socrates aliona jinsi vijana wa Athens walivyokuwa wakipotoshwa na masophisti. Akataka kuifanya kazi ya kifalsafa ya kuwatoa gizani watu wa Athens.

Maana, alibaini wale alioambiwa kuwa ni magwiji wa sheria katika Athens hawakuwa na maarifa hata ya misingi ya sheria.

Na wale alioambiwa kuwa ni magwiji wa kutunga mashairi katika Athens nzima, Socrates alibaini kuwa hawakujua hata misingi ya kutunga beti za mashairi.

Unafanyaje basi kuwageuza watu waliokuwa wakiamini katika walichokiamini? Kwamba Socrates ni nani kuwaambia watu wa Athens kuwa wale waliodhani kuwa wanajua hawakuwa na walijualo.

Na kama Socrates angekuwepo kwenye mkusanyiko huo wa watu hapo Mtaa Livingstone na Mkunguni, sijui angeanzia wapi kuwaambia wanaodhani kuwa wana maarifa ya sheria za barabarani na hata kujivalisha majukumu ya kuwa mahakimu na mawakili , kwamba , kwa kuanzia, kuwa mkusanyiko huo ni wa kimakosa kwa mujibu wa sheria.

Wote hao pichani hawakupaswa kuwa hapo, maana , si tu ni katikati ya barabara, bali wameingilia kazi ya trafiki wa barabarani, na pengine hawajui hata misingi ya sheria, ikiwamo sheria za barabarani!
Kuishi jirani na mahakama si kujua sheria.
Ni Neno La Leo.
Maggid,
Iringa.

About Muhammed Khamis

hosearevocatus9@gmail.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *