habari

Neno La Leo

By

on

Neno La Leo: Wasadikika Huitafuta Fimbo Baada Ya Kuumwa Na Nyoka..!

Ndugu zangu,

Shaaban Robert anaandika;

” Wasadikika wana desturi ya kuitafuta fimbo baada ya kuumwa na nyoka. Tumekwisha umwa na nyoka kwa matendo yetu mabaya ya zamani.

Nyoka mwenyewe amekwishakimbia. Hapatikani kwa kujilipiza kisasi, lakini, sumu yake imebakia katika jeraha tulilolipata. Sasa, shauri lililo jema ni kuzuia sumu hii isienee miilini mwetu ikaleta kifo.

Maovu yana hatari kubwa kukaa kati yetu. Tumedumu nayo kwa muda mrefu. Hayakutuletea faida ila hasara, huzuni na kilio siku zote.”- Shaaban Bin Robert.

Nyongeza hapa kwa aliyoyaandika Shaaban Robert, ni kwamba,
kihistoria Wasadikika huwa na hulka ya kufanya mzaha kwanza, kisha huamka dakika za mwisho. Hata kama ni mzaha wenye hatari ya kupelekea maangamizo ya taifa lao la Kusadikika.

Ona sasa wenzao akina Sadiki, wenye kuhamasisha taifa la Kusadikika lifuate mkondo wa mataifa mengine ambayo watu wake walichinjana kwa vile viongozi wao walikosa busara na hekima ya kukaa pamoja kuzimaliza tofauti zao kwa mazungumzo.

Na ajabu ya Nchi ya Kusadikika, walikubaliana kwanza watumie demokrasia ya masunduku ya kura kwenye kuwapata watawala wao. Lakini, kuna ambao wenye kuonyesha kukata tamaa ya kuyapata madaraka kwa kupitia demokrasia ya masanduku ya kura.

Hata kama kwenye Nchi Ya Kusadikika demokrasia ya masanduku ya kura ina mapungufu yake, busara na hekima ilipaswa kwa viongozi wenye kutawala na wapinzani wao, kukaa pamoja na kuzungumza namna bora ya kuimarisha demokrasia yao hiyo. Na zaidi, kwa kutumia ushawishi wa nguvu za hoja.

Kuchagua njia ya vurugu na machafuko kuyapata au kubaki kwenye madaraka, kamwe hakutaiacha salama Nchi Ya Kusadikika. Tumeshaziona Ishara.

Ni Neno La Leo.

Maggid.

About mjengwa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *