habari

Oparesheni Nzagamba Yang’oa Watumishi Wanne

on

Na Frank Mvungi- MAELEZO
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina ameagiza Kuondolewa mara moja kwa watumishi wa Wanaosimamia Kituo cha Ukaguzi Kibaha Mkoani Pwani kwa kushindwa kusimamia rasilimali za Sekta ya Mifugo na Uvuvi. Akizungumza leo Jijini Dodoma wakati  wa kikao cha Tathmini ya Operesheni Nzagamba Awamu ya Pili iliyofanyika  kati ya mwezi Oktoba na Novemba 2018 ikilenga Kuinua mchango wa Sekta ya Mifugo katika Pato la Taifa Waziri Mpina amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali yatokanayo na biashara ya Mifugo na Mazao yake.

“ Watumishi wote walioshiriki katika Operesheni Nzagamba Awamu ya Pili wamefanya kazi kubwa na kwa uzalendo mkubwa hivyo nawapongeza kwa kuwa mmeonesha kuwa tunao uwezo wa kusimamia rasilimali zetu ili zitoe mchango stahiki katika pato la Taifa”.Alisisitiza Mhe. Mpina. Akifafanua amesema watumishi wasio waadilfu na wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao hawana nafasi katika Wizara hiyo ndio maana ameagiza kuondolewa mara moja kwa watumishi wanaofanya kazi ya ukaguzi wa rasilimali hizo katika kituo cha Kibaha.
Aliongeza kuwa Operesheni Nzagamba awamu ya Pili, 2018 imedhihirisha kwamba usimamizi thabiti wa Sheria, Kanuni na Taratibu katika Sekta ya Mifugo unaweza kuleta tija kwa kuongeza uzalishaji bora wa mazao ya mifugo ambayo ni malighafi ya Viwanda na hivyo kuchangia ipasavyo katika kuendeleza uchumi wa Viwanda.

“ Ni mategemeo yangu kuwa wananchi mtakuwa wazalendo kwa nchi yetu kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za Kufanya biashara ya mifugo pia kutoa taarifa pale mnapobaini utoroshaji wa mifugo kwenda nchi jirani bila kulipiwa ushuru na tozo stahiki ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya watu hao”. Alibainisha Mhe. Mpina. Pia aliwaasa Watumishi wa Wizara hiyo na wale wa Halmashauri kuhakikisha kuwa wanasimamia kwa makini utekelezaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu zote zinazosimamia biashara ya Mifugo na Mazao yake hususan mabadiliko ya Kanuni mpya iliyotolewa mwezi Agosti, 2018.

Katika kuhakikisha minada yote ya awali na ile ya Upili pamaoja na ile ya mipakani inatoa matokea chanya, Waziri Mpina amesema kuwa  usimamizi utaendelea kuimarishwa ili kuwezesha biashara ya mifugo kufanyika kwa ufanisi na hivyo kurahisisha ukusanyaji wa maduhuli, tozo na ushuru wa Serikali. Alizitaka Mamlaka zinazotoa Leseni kwa wafanyabishara wanaosafirisha Mifugo nje ya nchi kuweka utaratibu rafiki utakaosaidia  kundi hilo kutoa mchango wake katika ujenzi wa Taifa na kuondoa au kupunguza vitendo vya biashara ya magendo. Aidha Waziri Mpina aliagiza kufunguliwa kwa Ofisi za Kanda ili kuimarisha usimamizi wa rasilimali za mazao ya mifugo hapa nchini.

Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kuwa Operesheni hiyo ilishirikisha watendaji 152 waliogawanyika katika timu 14 zilizofanya kazi katika nchi nzima. Akizungumzia mafanikio ya Operesheni hiyo amesema kuwa kwa mfano katika Mji wa Bunda zilikuwa zikikusanywa shilingi milioni mbili na nusu  (2.5) hapo awali ambapo kwa sasa baada ya kuimarisha ukusanyaji mapato katika eneo hilo yamefikia milioni nane  (8)kwa siku.

Udhibiti wa Biashara ya Mifugo na Mazao yake uliofanyika kupitia Operesheni Nzagamba II kuanzia tarehe 11 Oktoba, 2018 hadi tarehe 30 Novemba, 2018 (siku 50) umeiwezesha Wizara yangu kupitia Sekta ya Mifugo kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 5,773,074,768. Makusanyo haya yanapelekea Wizara hiyo katika sekta ya Mifugo tu kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 9,764,241,926.28 kwa kipindi cha Julai hadi Novemba, 2018 sawa na asilimia 52.87 ya lengo lililowekwa na Wizara ya Fedha.

About Muhammed Khamis

hosearevocatus9@gmail.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *