habari

Polisi Mmoja Kenya Ahukumiwa Miaka 15 Jela Kwa Mauaji.

on

Mahakama nchini Kenya imemhukumu afisa mmoja wa polisi nchini humo kutumikia kifungo cha miaka 15 jela baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya mwaka 2013 ya mwanaume aliyeshukiwa kuiba simu ya mkononi.

Polisi huyo, Titus Musila alipatikana na hatia mwezi Machi ya kumpiga risasi tatu za kichwani mshukiwa Kenneth Mwangi badala ya kumkamata.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, huo ni ushindi mkubwa kwa taasisi huru ya IPOA inayochunguza makosa yanayofanywa na polisi nchini Kenya. Kwa upande wa wachambuzi wanadai Polisi wa Kenya wamekuwa wakilaumiwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu pamoja na raia kutokana na mauaji ya kiholela lakini mara nyingi wamekuwa hawachukuliwi hatua au kufunguliwa mashtaka.

Wakati akitoa uamuzi huo, Jaji wa Mahakama Kuu James Wakiaga amesema kuwa uamuzi huo ni onyo kwa maafisa wa usalama wanaotumia silaha vibaya.

Hukumu hiyo ambayo wakili wa Musila, Cliff Ombeta amesema atakata rufaa, inakuwa ni mara ya pili kwa afisa wa polisi kupatikana na hatia na kufungwa jela kutokana na uchunguzi uliofanywa na IPOA ambayo ilianzishwa na serikali mwaka 2011, baada ya polisi kulaumiwa kwa kuhusika na vifo vya makumi ya waandamanaji katika vurugu zilizofuatia uchaguzi wa urais uliofanyika mwaka 2017, uliogubikwa na utata.

Polisi walikuwa wametuhumiwa kwa kutumia nguvu za ziada dhidi ya waandamanaji kufuatia uchaguzi wa mwaka 2017. IPOA ambao ni waangalizi, ni chombo ambacho kinaendeshwa na raia, kilichunguza kifo cha Mwangi baada ya ndugu zake kupeleka malalamiko dhidi ya afisa polisi huyo.

Hata hivyo juhudi za kupata maelezo ya polisi kuhusu hukumu hiyo ziligonga ukuta baada ya msemaji wa polisi Charles Owino kutopokea simu siku ya Alhamisi.

Mwaka 2016, maafisa wawili wa polisi walihukumiwa kwenda jela miaka saba baada ya mtoto wa kike wa miaka 14 kupigwa risasi katika msako uliofanyika katika nyumba mmoja Wilaya ya Pwani, Kaunti ya Kwale mwaka 2014.

Na VOA.

About Hosea Revocatus

hosearevocatus9@gmail.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *