habari

RC Iringa awaomba wadau wa utalii kuwekeza Nyanda za juu Kusini

on


MKUU wa mkoa wa Iringa Bi Amina Masenza akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam leo kuhusiana na Maonesho ya Utalii Karibu Kusini 2018 yanayotarajiwa kufanyika mkoani Iringa Septemba 26 hadi 30 mwaka huu. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Bw Richard Kasesela pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri Wilaya ya Iringa Bw. Robert Masunya. Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Bw Richard Kasesela (kushoto) akizungumza kwenye mkutano huo.
Mkurugenzi Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Ernest Mwamwaja (kulia) akizungumza kwenye mkutano huo.
Mratibu wa Maonesho ya Utalii Karibu Kusini 2018 kutoka Kampuni ya Capital Plus Internantional (CPI) Bw Clement Mshana (katikati) akizungumza kwenye mkutano huo. Kampuni hiyo inashirikiana na Mkoa wa Iringa kuratibu maonesho hayo.

MKUU wa mkoa wa Iringa Bi Amina Masenza (katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa mkoa huo pamoja na wadau kutoka TTB pamoja na Capital Plus Internanational

MKUU wa mkoa wa Iringa Mh. Amina Masenza ametoa wito kwa wadau wa utalii na maendeleo nchini kuwekeza zaidi kwenye sekta ya Utalii katika Ukanda wa Nyanda za juu Kusini ili kuunga mkono adhma ya serikali ya kufungua na kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana katika kanda hiyo.

Bi. Masenza ametoa wito huo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na Maonesho ya Utalii Karibu Kusini 2018 yanayoenda sambamba na Maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani Kitaifa yanayotarajiwa kufanyika mkoani Iringa Septemba 26 hadi 30 mwaka huu.

Alisema kwa sasa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini imejipanga kimkakati kuhakikisha kwamba inatangaza na fursa na vivutio vya kiutalii vinavyopatikana katika mikoa hiyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais John Pombe Magufuli alilolitoa hivi karibuni wakati wa kilele cha sherehe za Mei Mosi zilizofanyika kitaifa mkoani Iringa ambapo aliitaka mikoa hiyo kufunguka kiutalii.

Mikoa inayounda kanda hiyo ni pamoja na Iringa, Mbeya, Njombe, Songwe, Ruvuma, Rukwa na Katavi.

“Mikoa ya nyanda za juu Kusini inasifika kuwa na hifadhi zenye sifa za kipekee ikiwemo Taifa ya Ruaha yenye makundi makubwa ya tembo na wanyama wengine. Hifadhi nyingine ni Kitulo yenye aina mbali mbali za maua ambayo hayapatikani mahali pengine Duniani; na Udzungwa yenye wanyama adimu duniani kama vyura wa Kihansi na mengine mengi,’’ alitaja.

Akizungumzia maonesho hayo Bi Masenza alisema tofauti na miaka miwili iliyopita maonesho ya mwaka huu yataambatana na nyongeza ya matukio kadhaa ya kimichezo, kitaaluma na kiutamaduni ili kuongeza tija zaidi katika kufikia malengo ambayo hasa ni kuongeza mazao ya utalii katika kanda hiyo. “Mbali na maonyesho yenyewe kutakuwa na Kongamano la kujadili masuala ya Utalii na Uchumi litakalofanyika tarehe 27 Septemba, 2018, pia tutakuwa na matukio ya kimichezo ikiwemo Mashindano ya mchezo wa Golf yanayotarajiwa kufanyika Wilayani Mufindi kuanzia Julai 27 hadi 29, 2018,’’ alitaja.

Alitaja matukio mengine kuwa ni pamoja na Mashindano ya mbio za baiskeli, ngoma za asili, huku kilele cha maonesho hayo kikitarajiwa kupambwa na na Mashindano ya mbio za nyika (marathon). Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Bw Richard Kasesela alisema katika kipindi chote cha maonesho hayo umeandaliwa utaratibu wa usafiri kwa washiriki, wageni pamoja na wenyeji wa Mkoa Iringa ili waweze kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo katika ukanda huo

“Nawaomba sana wananchi wote wajipange kushiriki katika maonesho haya makubwa. Pia niwaombe sana wadau wetu wa maendeleo ikiwemo sekta binafsi wajitokeze kwa wingi kuunga mkono maonesho haya.’’ Alisema

Naye Mkurugenzi Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Ernest Mwamwaja alisema kwasasa bodi hiyo imejipanga vyema kuhakikisha kwamba inawekeza nguvu zaidi katika kutangaza utalii wa Nyanda za Juu Kusini ili kuleta uwiano wenye afya kiutalii hapa nchini. “TTB tumekuwa tukishiriki kwenye maonyesho mbalimbali ya kitalii ndani nan je ya nchi hivyo basi kwenye mkakati huu jukumu letu kubwa litakuwa ni kusambaza ujumbe kwa wadau wote ndani na nje ya nchi kuhusiana na fursa pamoja na vivutio vya utalii katika Nyanda za Juu Kusini,’’ alisema.

Mratibu wa maonesho hayo kutoka Kampuni ya Capital Plus Internantional (CPI) inayoshirikiana na Mkoa wa Iringa kuratibu maonesho hayo, Bw Clement Mshana alisema kwa mwaka huu yana maboresho makubwa ambapo mbali na kuongeza uhusishwaji wa sekta binafsi wao, kama waratibu wamejipanga kuhakikisha yanaandaliwa katika viwango vya kimataifa.

About Muhammed Khamis

hosearevocatus9@gmail.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *