We have 160 guests and no members online

Posted On Saturday, 24 October 2015 03:40

Vijana Kisiwanin Pemba wakiingia katika viwanja vya Gombani kuhudhuria Mkutano wa Ufungaji wa Kampeni ya CCM ya Mgombea Urais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein.

Wanachama wa CCM wakiwa katika viwanja vya Gombani ya Kale Pemba wakihudhuria mkutano wa kampeni ya Mgombea Urais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Balozi Seif Ali Iddi akiwasili katika viwanja vya mkutano wa ufungaji wa kampeni katika viwanja vya Gombani ya Kale akisalimiana na Viongozi wa CCM Pemba.

Mgombea Mwenza wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokelewa na Naibu Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar Mhe Salama Aboud Talib.akiwasili katika viwanja vya mkutano Gombani ya Kale. Pemba.

Mgombea Mwenza wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ziwani Pemba Ndg Mohammed Othman Omar alipowasili katika viwanja vya mkutano.(P.T)

Posted On Friday, 23 October 2015 10:03

Merkel na Netanyahu

Netanyahu alidai Hitler mwanzoni hakutaka kuwaangamiza Wayahudi

Ujerumani imesisitiza kwamba ndiyo inayowajibika kwa mauaji ya Wayahudi wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Hii ni baada ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuibua mzozo mkubwa baada yake kudai kiongozi mmoja wa Wapalestina ndiye aliyewaambia viongozi wa chama cha Nazi kuwaua Wayahudi barani Ulaya.

Chansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema Wajerumani wanafahamu wazi kwamba viongozi wa Nazi ndio waliopanga na kutekeleza mauaji hayo yajulikanayo kama Holocaust.

Netanyahu alikuwa amedai kiongozi wa Nazi Adolf Hitler alitaka tu kuwafurusha Wayahudi kutoka Ulaya, lakini Mufti Mkuu wa Jerusalem Haj Amin al-Husseini akamwambia: "Wachome moto."

Posted On Friday, 23 October 2015 04:17

Hillary Clinton

Anayedhaniwa kuwa mstari wa mbele katika uteuzi wa Urais katika chama cha Democratic, Hillary Clinton, amewalaumu wapinzani wake wa chama cha Republican kwa kutumia vifo vya wanadiplomasia nchini Libya kujinufaisha kisiasa.

Bi Clinton amekuwa akitoa ushahidi mbele ya Kamati ya Bunge la Congress inayochunguza shambulizi katika ubalozi wa Marekani nchini Libya, katika mji wa Benghazi mwaka 2012 alipokuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni.

Alisema alijiwajibisha kwa kukubali kosa hilo ambapo watu wanne walifariki, kukiwemo balozi Christopher Stevens.

Mwanachama mkongwe wa kamati huyo kutoka chama cha Democratic, Elijah Cummings, alisema kuwa uchunguzi huo unaoongozwa na chama cha Republican ni matumizi mabaya ya sheria yenye lengo la kumvurugia Bi Clinton kampeni yake ya kutaka kuwa Rais wa Marekani.BBC

Posted On Friday, 23 October 2015 04:16

 

Posted On Friday, 23 October 2015 04:15

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na Mjumbe wa Kamati ya Kampeni, January Makamba.

CCM itafunga kampeni zake kwa utaratibu mpya na kwa kishindo. Kampeni za CCM zitafungwa kitaifa kwa mikutano mikubwa ya kampeni katika mikoa mitano. Mikutano hiyo itaongozwa na viongozi wa CCM kitaifa waliopo madarakani na wastaafu. Mikoa hiyo na viongozi wakaoongoza mikutano hiyo ni kama ifuatavyo:

1. Mwanza – Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete, Mwenyekiti wa CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, Mgombea Urais, na Ndugu Samia Hassan Suluhu, Mgombea Makamu wa Rais

2. Tanga – Ndugu Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM

3. Mbeya – Ndugu Benjamin William Mkapa, Mwenyekiti wa CCM Mstaafu

4. Mtwara – Ndugu Ali Hassan Mwinyi, Mwenyekiti wa CCM Mstaafu

5. Kigoma – Ndugu Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM

6. Kilimanjaro – Ndugu Yusuf Makamba, Katibu Mkuu wa CCM Mstaafu

7. Mara – Ndugu Joseph Warioba, Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu Mstaafu

Kati ya leo na kesho, maeneo mengine yanaweza kuongezeka. Mikutano hii itaanza saa sita mchana na itarushwa, yote kwa pamoja, kwa matangazo ya moja kwa moja ya vituo vya televisheni vitano na vituoa vya redio 67. Vilevile, watakaohudhuria katika mikutano hii wataunganishwa moja kwa moja na mkutano wa Mwanza, alipo Mwenyekiti, Mgombea na Mgombea Mwenza, na wataweza kusikiliza hotuba ya Dkt. Magufuli moja kwa moja kupitia screens zitakazokuwa katika viwanjani vyote hivi saba.

Namna hii ya ufungaji wa kampeni itakuwa ni ya kihistoria, na inadhihirisha nguvu ya CCM inayoiwezesha kufanya mikutano mikubwa ya kampeni kwa siku moja katika maeneo mbalimbali nchini. Lakini pia tutafanya historia katika tasnia ya utangazaji wa televisheni hapa nchini kwa kutangaza na kuunganisha kwa pamoja matukio saba kwa wakati mmoja.

Kwa upande wa Dar es Salaam, tutafanya mkutano mkubwa wa ufungaji wa kampeni za Mkoa wa Dar es Salaam, katika Uwanja wa Jangwani, kesho, Ijumaa, tarehe 23 Oktoba 2015. Siku ya Jumamosi, tarehe 24 Oktoba 2015, Wagombea Ubunge katika majimbo ya Mkoa wa Dar es Salaam watafunga kampeni katika maeneo ya majimbo yao kwa namna mahsusi.

Tathmini ya Kampeni Kama Chama, tumeridhika na ubora na ukubwa wa kampeni tulizofanya licha ya changamoto za hapa na pale. Dkt. Magufuli na Ndugu Suluhu wamefanya kazi kubwa, na kwa bidii kubwa, na maarifa makubwa. Wamekuwa barabarani kwa siku 57 wakifanya mikutano kati ya 8 hadi 12 kwa siku. Imani yetu ya ushindi inatokana na kazi kubwa waliyofanya. Pia, CCM inawashukuru viongozi, wapenzi wa washabiki wake – wa makundi mbalimbali ya kijamii - kote nchini kwa kazi kwa kazi kubwa ya kampeni waliyoifanya.

Kutokana na kazi kubwa na nzuri iliyofanyika, na kutokana na mwenendo wa tafiti huru na tafiti zetu za ndani, CCM inategemea ushindi wa asilimia zisizopungua 69.

Uchaguzi wa Amani

CCM haitachoka kuendelea kusisitiza uchaguzi wa amani na utulivu. Sisi kama chama kikubwa cha siasa nchini, chenye wafuasi wengi zaidi, na chenye dhamana ya uongozi wa dola, tutatimiza wajibu wetu wa kuhimiza utulivu kwa wapenzi, washabiki na wanachama wetu. Tunawataka na wenzetu wafanye hivyo.

Kauli za wenzetu kwamba kura zitaibiwa ni kauli za kutojiamini na kujiandaa kufanya vurugu. Kauli za kwamba washabiki wa UKAWA wakishapiga kura wabaki vituoni kulinda kura si kauli za wanaotaka uchaguzi wa amani.

Kwa utaratibu wetu wa uchaguzi, utaratibu wa pekee kwa Chama kulinda kura zake ni kwa kupitia wakala wa vyama waliopo kwenye kila kituo cha kupiga kura na wenye nguvu na mamlaka ya kisheria ya kushuhudia zoezi zima, kuanzia kupiga kura, kuhesabu kura hadi kutangaza matokeo. Kura zinapigwa na kuhesabiwa vituoni mbele ya wasimamizi wa uchaguzi, mawakala wa vyama na waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje ya nchi.

Mawakala wa vyama na wasimamizi wa uchaguzi wanaweka sahihi kwenye fomu za matokeo, na matokeo hayo yanatangazwa na kubandikwa kwenye kituo. Kwenye kituo kikuu cha Tume cha kujumlisha matokeo, mawakala wa vyama pia huwepo na Tume hujumlisha matokeo kutoka kwenye fomu za matokeo za vituo vya nchi nzima zilizosainiwa na mawakala wa vyama kwenye kila kituo. Kwa viongozi wa UKAWA kuwaambia watu waingie barabarani au kuvizunguka vituo vya kupigia kura eti ili kulinda kura hakuna maana yoyote zaidi ya kutafuta namna ya kuhalalisha vujo, vurugu na uporaji na kuwazuia watu wengine, hasa wanawake, kupiga kura. Tunaviomba vyombo vya ulinzi na usalama vizuie hili jambo kwasababu halina nia njema.

Mkakati wa UKAWA ni kufanya vurugu baada ya kushindwa na kutengeneza mazingira ya mgogoro wa kisiasa ili Jumuiya ya Kimataifa iingilie kati na kupendekeza kugawana madaraka. Mkakati huo hautafanikiwa. Tunaviomba vyombo ya ulinzi na usalama vihakikishe ulinzi na usalama wa watu wote na mali zao siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi.

CCM haitakubali hata kidogo ushindi wake kuhojiwa au kutiliwa shaka kwasababu tu ya vurugu zilizoanzishwa na watu wengine.

Siku ya Jumamosi, CCM itatangaza namba maalum za simu kwa Watanzania wote ili siku kabla ya uchaguzi, siku ya uchaguzi na mara baada ya uchaguzi, waweze kupiga simu au kutuma ujumbe pale watakapokuwa wanabaini au kushuhudia vitendo vya kuvuruga amani na kuvuruga utaratibu mzima wa uchaguzi.

Kupokea Matokeo

CCM imeweka utaratibu wa kupokea matokeo kwa kutumia mawakala wake moja kwa moja vituoni na kupitia mtandao wa Chama. CCM inategemea kuwa na matokeo ya uchaguzi nchi nzima ifikapo saa nne usiku, siku ya uchaguzi, tarehe 25 Oktoba 2015.

Imetolewa na:

January Makamba
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni
22 Oktoba 2015(P.T)

Posted On Friday, 23 October 2015 04:13

0_244ec.jpg


Ndugu zangu,
Jana niliwaahidi kuwasimulia kilichotokea mwaka 1996. Jioni moja rafiki yangu, Balozi mmoja wa nchi ya Kimagharibi, kwa sababu za kidiplomasia, simtaji jina wala nchi anayotoka, alifika nyumbani nilikokuwa nikiishi, Kinondoni Biafra.
Alikuwa yeye na dereva wake tu. Tulipokaa kuongea akanieleza kuwa ametokea ofisi za TLP Manzese kufanya mazungumzo na Augustine Mrema katika yeye Balozi kuwafahamu viongozi wa upinzani na kuwasikiliza.
Akaniambia, kuwa walikubaliana na Mrema , kuwa ili kuepusha mgongano na Serikali ya Tanzania, ziara ile ya Balozi isifanywe kuwa rasmi na kutangazwa kwenye vyombo vya habari. Mrema kwenye mazungumzo alikuwa na wajumbe kadhaa wa chama chake.
Balozi yule katika kunisimulia kule nikamuuliza;
" Je, mazungumzo yenu yaliishaje?"
Rafiki yangu Balozi akaniambia walimaliza kwa kupiga picha ya pamoja ambayo Mrema aliitaka sana ipigwe. Balozi akarudia tena kuomba kuwa picha hiyo isitumike kwenye media. Mheshimiwa Balozi akaniambia kuwa alihakikishiwa kuwa hilo lisingetokea.
Rafiki yangu Balozi yule akanishangaa sana nilipomwambia kuwa asishangae picha hiyo ikawa kwenye kurasa za mbele kwenye moja ya magazeti siku inayofuata.
Siku ya pili yake, gazeti la Majira likachapisha picha ukurasa wa mbele ikimwonyesha Balozi akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa TLP kwenye ofisi za chama hicho Manzese na huku Augustino Mrema akiwa amejaa katikati ya picha kulia kwa Mheshimiwa Balozi wa Nchi Muhimu ya Kimagharibi!
Niliikata picha hiyo na kumtumia balozi yule, naye abaki na kumbukumbu ya tukio la Manzese, Tanzania!
Maggid.
Iringa.

Posted On Thursday, 22 October 2015 19:40

2_d4cb5.jpg


Ndugu zangu,
Nionavyo, Nchi yetu iko katika hali ya kama mgonjwa anayetafuta mawili makubwa; nafuu na uimara wa afya yake.
Kama upepo kinzani hautalizuia taifa letu katika kusonga mbele, basi, miaka ijayo itakuwa ni miaka ya ' Nchi kuanza kuwa na kukua zaidi' kutoka hali ya sasa. Nchi itarajie mabadiliko makubwa hata kwenye mitazamo yetu kuhusu kazi na nidhamu ya kazi hususan kwa watendaji.
Hata hivyo, kwenye hali ya mgonjwa kuelekea kuitafuta nafuu na uimara wa afya, uwezo , njia na mbinu za waganga zaweza kutofautiana. Uchaguzi ina maana pia ya kumtafuta yule mganga mwenye kuonyesha kuwa na uwezo, njia na mbinu za kuipata nafuu na uimara wa afya ya mgonjwa.
Hivyo, tukiwa sasa, kama taifa zima, na tunapoelekea kwenda kulijenga daraja kati ya jana na kesho, ni muhimu tukaitazama Tanzania kwanza na kuwa na mioyo ya kuvumiliana na kuheshimiana. Umuhimu wa kuilinda amani yetu.
Ndugu zangu,
Katika kuishi kwangu nina bahati ya kuwa na uzoefu wa miaka mingi wa kufuatilia siasa za kitaifa, bara la Afrika na dunia kwa ujumla.
Katika kuishi kwangu pia, sijawa na wala sifikirii kuja kuwa mwanachama wa chama cha siasa. Kwangu Watanzania wa vyama vyote, na wasio na vyama ni ndugu zangu. Na kwa kusema hivyo haina maana sina itikadi ya kisiasa inayoniongoza. Mimi naamini katika Ujamaa na Kujitegemea. Ndio, I am a Social Democrat.
Nilichokiweka mezani jana ni mtazamo wangu. Sijarudi nyuma hata robo hatua. Nimesimama pale pale, kwamba ninachokiona ni kuwa Serikali inayokuja ya Awamu ya Tano itaundwa na John Pombe Magufuli.
La Magufuli kuunda Serikali ishara zake niliziona muda mrefu na nikaweka bayana hilo mwezi uliopita. Na leo zikiwa zimebaki siku tatu kabla kufanyika Uchaguzi Mkuu, hakika sizioni ishara mpya.
Kwanini John Magufuli atashinda?
Kuna sababu moja kubwa. Kwamba wakati mgombea wa Ukawa- Chadema anabebwa na umaarufu aliokuwa nao akiwa CCM, umaarufu huo wa mtu mmoja umekuwa wa gharama kwa Chadema kama chama.
Ni kwa vile, ilitarajiwa, na haikutokea, kuwa mgombea urais wa Ukawa- Chadema angetoka CCM na kundi kubwa la wafuasi kutoka CCM. Kwa sasa wachache waliohama CCM na Edward Lowassa wako katika kundi la ' Political spent forces'. Ni waliokwishatumika kisiasa kwa sifa ya mazuri na mabaya.
Kabla ya kuhama kwao hawakuwa kwenye nafasi za juu kwenye chama na Serikali, na kuhama kwao kunaweza pia kutafsiriwa kuwa ' Wamechoshwa na masengenyo ya ndani ya chama'.
Kwamba chama chao kilishindwa kuwaonyesha umuhimu wao. Ndio, kumekuwa na kundi la ' Wanasiasa wanung'unikaji' ambao wangetimiziwa haja zao za kisiasa wangebaki huko huko CCM na wangesimama majukwaani kuimba ubora wa CCM !
Ni kweli kuwa, kwenye siasa umaarufu wa mgombea ni jambo muhimu, lakini, sadaka za kisiasa huambatana na umaarufu wa chama na kukubalika kwake kwa wananchi.
Kwa ajenda ya kupambana na ufisadi ambayo Ukawa- Chadema walikuwa nayo mpaka miezi kadhaa iliyopita, kimsingi iliwajengea umaarufu na kukubalika kama chama. Ni jambo la ajabu sana kuwa upinzani ukiongozwa na Chadema umeitupilia mbali ajenda hiyo.
Ziada ya matatizo ya upinzani kwa sasa ni hali ya kutoelewana kwa viongozi wakuu ndani ya upinzani. Hali ya hata kugombania majimbo na kata. Na kujiweka pembeni kwa Dr Slaa na Profesa Lipumba ni pigo kubwa.
Ina tafsiri ya upinzani kupoteza sehemu kubwa ya mtaji wa imani kutoka kwa wapiga kura. Upinzani umeshindwa kuonyesha mshikamano wa kiuongozi- Cohesive leadership.
Wapiga kura wanaelewa kuwa uongozi wa juu wa nchi ni jambo muhimu na nyeti. Linahusu mustakabali wa nchi na maisha yao. Kwa viongozi wa upinzani kushindwa kuonyesha cohesive leadership hakuwapi imani wapiga kura walio wengi kuwa mambo yatakuwa shwari watu hao hao wakipewa nafasi ya kuongoza nchi.
Na ujio wa Edward Lowassa Ukawa- Chadema umeliibua kundi lingine la ' Wanung'unikaji' ndani ya UKAWA. Hawa wanahoji taratibu za Lowassa kuingizwa Ukawa na kupewa nafasi ya juu ya kugombea urais. Ikumbukwe, Dr Slaa na Profesa Lipumba wamejiengua, nao wana wafuasi wao.
Watanzania huchagua zimwi..
Chama cha Mapinduzi katika Tanzania ni zaidi ya Chama cha siasa. Ni taasisi kubwa na karibu kila Mtanzania ana nasaba na CCM. Ni moja ya vyama vikongwe Afrika vyenye sifa kubwa ya kuwa na mizizi katika kila eneo la ardhi ya nchi wanakoishi watu. CCM ni sehemu ya maisha ya Watanzania.
Ni katika uhalisia huo, kuna wanaokipenda chama hicho na kuna wanaokichukia pia, kwa wenye kukichukia kwao ni zaidi ya zimwi, ni kama shetani anayewawekea giza kwenye maisha yao. Watu hawa hulilia mabadiliko, na kwao tafsiri ya mabadiliko ni kuiondoa CCM tu, basi. Hawa si wengi sana kama inavyodhaniwa, lakini, wana uwezo mkubwa wa kupiga kelele ambazo CCM hawapaswi kuzipuuzia.
Na hakika, katika kero na matatizo mengi wanayoyapata Watanzania, hufika mahali wapiga kura wengi wanajua kuwa wanakwenda kuchagua zimwi.
Kwa tabia, wapiga kura huwa ni waoga sana kuchagua wasichokijua. Na wanajua pia, kuwa Rais wa nchi ni nafasi nyeti. Kama hawawajui watakaomzunguka Rais, basi, huingiwa na mashaka.
Wahenga walisema; " Zimwi likujualo halikuli likakwisha". Hivyo, Wapiga kura wengi kwa tabia huenda kuchagua zimwi wanalolijua, na hapa ni CCM.
Edward Lowassa angehama na ' Mazimwi' mengi kutoka CCM, tena yale ambayo wapiga kura wanayajua, basi, nafasi ya Edward Lowasa kushinda urais ingekuwa kubwa.
Mimi naamini, Lowassa angebaki kuwa mgombea ndani ya CCM, bado Lowassa na CCM wangeshinda , lakini kwa tabu sana kwa mantiki ile ile ya mgombea kuzungukwa na mazimwi mengi ambayo wapiga kura wanayajua. Lakini, upinzani ungepata viti vingi zaidi kuliko ambavyo itapata kwenye uchaguzi ujao, ni kwa vile, upinzani ungebeba ajenda ya kupambana na ufisadi ambayo ni kero kubwa kwa Watanzania wengi. Na nchi yetu inahitaji siasa za upinzani kuanzia kwenye udiwani hadi ubunge.
Vinginevyo, kwa hali ninavyoiona sasa, Watanzania tutarajie ujio wa Serikali ya John Pombe Magufuli kama Rais wa Awamu ya Tano.
Ni mtazamo wangu.
Maggid,
Iringa.

Posted On Thursday, 22 October 2015 10:47

Ndugu zangu,

Naziona kila dalili, na nimelisema hili zaidi ya mwezi mmoja uliopita, kuwa mgombea urais wa CCM, John Pombe Magufuli ndiye atakayeunda Serikali ijayo ya Awamu ya Tano. Na sasa naiona pia shaka moja kubwa katika utawala ujao wa John Magufuli. Ni shaka ya kweli na naamini ndiyo kimsingi imetufikisha hapa tulipo leo.

Kwenye kampeni zake, John Magufuli amefaulu kuibeba ajenda ya kupambana na rushwa na ufisadi. Kupambana na watendaji wazembe. Kati ya nyingi, ukweli hizo ndio kero kubwa za Watanzania. Ni bahati mbaya kwa UKAWA ikiongozwa na Chadema, kuwa hii ndio ilikuwa ajenda yao waliyoibeba huko nyuma , nayo ikawabeba kisiasa. Wameipoteza, hivyo kupoteza pia dira kisiasa. Zikiwa zimebaki siku nne tu kabla ya Watanzania kupiga kura, ni miujiza tu ya kisiasa itakayopelekea Ukawa waliopoteana kurudi kwenye reli kuu na kupewa na wapiga kura, dhamana ya kuunda Serikali.

Na kwa hakika, ujio wa John Magufuli utaambatana na matarijio makubwa ya umma juu yake. Shaka kuu inajengwa na swali la je, atakidhi matarajio hayo katika mazingira ambayo yamepelekea Chama chake kuwa mbali na wanyonge kwa kukubali wafanyabiashara kuwa karibu sana na chama, na pengine hata baadhi ya viongozi wa dini ? Na bahati mbaya umma hautataka kusubiri mwezi mmoja upite, utataka kusikia kwa kauli na matendo utekelezaji wa yale ambayo John Magufuli amekuwa akiyahubiri kwenye majukwaa ya kampeni.

John Magufuli anayekuja, atakuwa na nafasi ya kipekee inayofanana na ya Mwalimu Nyerere kwa kuweka rekodi ya kuingia madarakani kwa kufanya kampeni ambazo hazikuhusisha sana matumizi makubwa ya fedha ambayo mara nyingi huambatana na michango ya wafanyabiashara wakubwa. Hivyo, John Magufuli hatakuwa na wadeni wake wa kuwalipa fadhila, isipokuwa, kuwahakikishia wafanyabiashara hao, uwepo wa mazingira mazuri ya kufanya biashara zao na walipe kodi ili zisaidie maendeleo ya wananchi wengine walio wengi. Kuna haja ya kutenganisha biashara na siasa, kuwa hata watendaji wakiwamo mawaziri, mbali ya Magufuli kuwasainisha mikataba, lakini umma ungetaka pia kwenye mikataba hiyo mawaziri na watendaji wakuu wawe tayari kutenganisha uongozi wa kisiasa/utendaji wa kiserikali na shughuli zao za kibiashara.

Na kwa kweli hili za kampeni za urais kuchangiwa na wafanyabiashara wakubwa lina mifano hai ya athari hata kwa wenzetu walioendelea kidemokrasia mfano wa Marekani.

Kwenye kampeni za kuwania Urais wa Marekani mwaka 1996, ambapo, mbali ya Bill Clinton kupambana na George Bush ( Baba) alikuwepo mgombea binafsi bilionea Ross Perrot aliyegharamia kampeni za urais wake kwa fedha za mfukoni mwake. Wamarekani hawakuwa tayari kutawaliwa na Rais bilionea Ross Perrot, na pamoja na ushindi wa Bill Clinton, Wamarekani walitilia shaka pia michango aliyopewa Bill Clinton na wafanyabiashara wakihofia kuwa wafanyabiashara hao wangenufaika zaidi kwa misamaha ya kodi. Katika hili, Bill Clinton mwenyewe, mwaka ule wa 1996, alikiri udhaifu huo kwa kutamka;

" Mistakes were made in raising money for my re-election campaign, but contributors did not buy influence with me and the system is not corrupt.." ( Mwandishi, The Guardian, Juni 30, 1996)

Tafsiri hapo ni kuwa, Clinton alikiri kuwa makosa yalifanyika katika kuchangisha fedha kumwezesha kushinda awamu ya pili ya urais, lakini, wachangiaji wa fedha hawakuweza kununua ushawishi kwake na kwamba mfumo haujaathirika na rushwa/ufisadi.

Kimsingi, katika nchi zetu hizi, hatari ya Rais na chama cha siasa kutokuwa na mipaka inayoonekana wazi yenye kutenganisha siasa na biashara, ina matokeo ya rais aliye madarakani na chama husika, kuwa mbali na wanyonge walio wengi.

Kuna wakati, akiwa madarakani, Benjamin Mkapa aliwaambia wazi wana CCM wenzake kule Dodoma, kuwa kihistoria, TANU na CCM imekuwa kimbilio la wanyonge. Mkapa akabainisha, kuwa CCM ya sasa inakimbiliwa na wafanyabiashara. Hili ni kosa la kisiasa.

Na nilipata kuandika, kuwa kama Chama Cha Mapinduzi kina nia ya kupunguza kupotea kwa imani ya umma kwa chama hicho, basi, kutahitajika, si tu kufanyika mabadiliko makubwa ndani ya muundo wa Serikali na uongozi wa Chama Cha Mapinduzi, bali kufanyika kwa mabadiliko makubwa yenye kishindo. Moja ya matarajio ya umma sasa, sio tu Wana-CCM, ni kuwa kwenye urais wake, John Magufuli ataongoza mabadiliko hayo makubwa na ya kishindo.

Kuna watakaopuuza, lakini, ni ukweli, kuwa tuhuma za ufisadi zimekipaka matope mno Chama Cha Mapinduzi. Kwenye macho ya umma, chama hicho kimechafuliwa na tuhuma hizo za ufisadi. John Magufuli ni ' kofia mpya' kiutawala. Jumapili ijayo, kwa hali ilivyo sasa, Watanzania watakwenda kuchagua ' Kofia Mpya'. Hivyo, watakuwa na matarajio makubwa yanayoweza kugeuka anguko kuu la Magufuli na CCM kwa chaguzi zijazo, kama Magufuli asipotimiza matarajio hayo.

Na matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu yawe ni fundisho kwa chama tawala. Kama CCM itataka kubaki kwenye mioyo ya Watanzania wengi, kuwa na uhalali wa kubaki madarakani, basi, ina lazima ya kujipambanua kwa vitendo kutoka kwenye yote makubwa yenye kuhusiana na ufisadi na maovu mengine. Ibaki kuwa kimbilio la wanyonge. Isifike mahali, chama kikajikuta katikati ya mgogoro na umma. Hilo laweza kuharakisha mazishi ya chama hicho, yasiyo na kisomo.

Maggid,
Iringa.(P.T)

Posted On Wednesday, 21 October 2015 09:40

Mbunge wa jimbo la Moshi mjini aliyemaliza muda wake ,Philemoni Ndesamburo,akimnadi mgombea Ubunge katika jimbo hilo Jafary Michael (Chadema) katika mkutano wa kampeni uliofanyika jana katika kata ya Ngangamfumuni.

Baadhi ya wananchi wakiwa kando ya barabara wakifuatilia mkutano huo.

Mgombea Ubunge jimbo la Moshi mjini kupitia Chadema,Jafary Michael akiomba kura wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika kata ya Ngangamfumuni mjini Moshi.

Mwenyekiti wa Chadema na mbunge anayemaliza muda wake katika jimbo la Moshi mjini,Philemoni Ndesamburo (katikati) akiwa na mgombea udiwani kata ya Ngangamfumuni,Anthony (kulia ) na mgombea udiwani kata ya Longuo Raymond Mboya. (kushoto).(P.T)

Posted On Tuesday, 20 October 2015 05:37

Mgombea ubunge kwa tiketi ya ccm jimbo la kibamba dkt Fenella Mukangara

 wananchi wakimsikiliza Mgombea ubunge kwa tiketi ya ccm jimbo la kibamba dkt Fenella Mukangara.

Na Jimmy Kagaruki,Kibamba

Mgombea ubunge kwa tiketi ya ccm jimbo la kibamba dkt Fenella Mukangara amesema atalifanya jimbo hilo kuwa la kisasa kwa muda wa miaka mitano ijayo.


Dkt fenella ameyasema hayo kwenye mkutano wa kampeni za ubunge jimbo la kibamba kwenye kata ya saranga.

Akihutubia mamia ya wananchi wa kata hiyo dkt fenella amesema akichaguliwa katika kipindi cha miaka mitano atakabikiana na changamoto za kiuchumi ikiwemo ukosefu wa ajira, miundombinunha barabara, elimu na afya 

Kuhusu chanhamoto ya ajira dkt fenella amesema atahakikisha anazalisha ajira kwa vijana na akina mama kwa kuwaweka kwenye vikundi vya nguvu kazi iki wapate mitaji na iwe rahisi kwao kukopoesheka.

Ameonbeza musema kuwa atahakikisha anaanzisha mtandao wa mawasiliano jimboni humo ikiwemo kituo ca radio ya jamii ( kibamba fm ) ambacho kitakua kiunganishi madhubuti kwa wananchi wa jimbo la kibamba. " najua wananchi wa kibamba mna kiu na shauku ya kuwa na njia ya kuoaza sauti zenu, nawaahidi nitaanzisha radio yenu kibamba fm ambayo itatusaidia kisikuma maendeleo yetu mbele na hata kuzalosha ajira"


Dkt fenella amesisitiza wananchi wa jimbo hilo wasifanye makosa kiwachagua wapinzani bali wachague wagombea wote kutoka ccm ili wapate maendeleo ya kweli.(P.T)

Posted On Tuesday, 20 October 2015 05:35

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano kwa Tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli, akielekea katika makaburi ya makaburi ya babu na bibi yake mzaa wa baba, eneo la Katoma, wilayani Geita Vijijini huku akiwa ameambatana na ndugu zake ikiwemo baba zake wadogo na mama zake wadogo.

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano kwa Tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli, akiwa katika makaburi ya makaburi ya babu na bibi yake mzaa wa baba, eneo la Katoma, wilayani Geita Vijijini akiwatambulisha ndugu zake ikiwemo baba yake mdogo, Michael Magufuli.(P.T)

Posted On Tuesday, 20 October 2015 04:46
Page 6 of 116

Tafuta Habari

Blog Shabihana

Znateli