We have 148 guests and no members online

mjengwablog

mjengwablog

Sunday, 18 February 2018 07:37

Neno La Leo: Yesu Na Kipofu Yule Wa Yeriko..

 

Ndugu zangu,

Imeandikwa kwenye vitabu vitakatifu, Marko 10:46-52 
Yesu alipokuwa akiondoka Yeriko pamoja na Wanafunzi wake akatokea kipofu, jina lake Barti mayo. Kipofu huyu alikuwa ameketi kando kando ya njia, akiomba.

Kipofu yule alipomwona Yesu akapiga kelele;

“Yesu, Mwana wa Daudi, nionee huruma!”

Naye Yesu akasimama na akamwambia;

“Unataka nikusaidie nini?”

Ni nini basi tafsiri ya swali hili la Yesu kwa kipofu yule Barti Mayo?

Jibu:

Yesu hakutanguliza dhahania ( Speculation), kuwa kipofu yule alichotaka ni kuona. Kikubwa kuliko vyote kwa mwanadamu ni UPENDO. Yesu alionyesha upendo wa hali ya juu kwa kipofu yule kwa kuanza na kumwuliza; " Unataka nikusaidie nini?"

Moja ya vilivyo na upendo mkubwa kwa mwanadamu kuvitenda kwa mwanadamu mwenzake ni kuuliza na baadae kusubiri jibu.

Ni hulka mbaya ya mwanadamu kutumia muda mwingi kujitanguliza mwenyewe. Kuzungumza juu ya yenye kumhusu na zaidi kujisifia. Hapo mwanadamu husahau kuuliza na kusikiliza.

Kama viongozi, mengine yanayotokea kwenye jamii yanatutaka tuanze na kuuliza, kisha tuyasikilize kwa kina majibu yanayotolewa na tunaowaongoza. Kisha, tuyafanyie kazi. Tusiyanyamazie.

Maana, Martin Luther alipata kutamka;

"Our lives begin to end the day we become silent about things that matter."- Martin Luther King Jr.

Ni Neno La Leo.

Maggid.

 

 

 

 

Image may contain: outdoor

 

Ndugu zangu,

Mwanafalsafa Jean- Paul Sartre anasema; “ Hell is the other people” – Kwamba jehanam ni wale wengine. Anataka pia tukubaliane, kuwa pepo yaweza kuwa ni wale wengine.

Na hakika, tofauti ya mwanadamu na mnyama iko kwenye kufikiri. Mnyama anaongozwa na hisia, lakini mwanadamu anapaswa aongozwe na kufikiri. Ndio maana ng’ombe anaweza kumpanda mama yake. Ni hisia tu zitakazoongoza tendo lake.

Hivyo, mwanadamu kwenye mambo ya msingi hapaswi
kabisa kuongozwa na hisia ikiwamo ushabiki. Anapaswa kufikiri. Na zaidi kufikiri kwa bidii.

Vinginevyo, ni ukweli, kuwa kijamii, mwanadamu anaweza kuwa kiumbe anayeishi kwenye mahusiano ya kirafiki na kiadui na wenzake. Na katika hilo la uadui, wanadamu, kama ilivyo kwa wanyama, wanaweza kushindania na hata kugombania vingi; iwe fedha, mashamba, mapenzi na hata kivuli cha mti.

Ndio, unaweza kabisa kuwakuta wanadamu wawili wanagombania kivuli cha mti, kwamba nani mwenye haki ya kukaa kivulini. Na wanaweza kugombana mpaka akatokea mwendawazimu atakayekuja kuukata na huo mti wenyewe. Na wanadamu hao watabaki wakitazamana juani.

Mara nyingi, migogoro husababishwa na kugombania kisichotosha. Hivyo, lililo la msingi ni kutambua, kuwa wanadamu tunategemeana. Kwamba panapo kushindania jambo, mwanadamu, tofauti na mnyama, anapaswa kufikiri sana. Atangulize kwanza hekima na busara.

Na kwenye mgogoro wowote ule, mwanadamu ayape mazungumzo nafasi ya pekee katika kufikia muafaka, na si vurugu au mapigano. Kwenye mgogoro, na kwenye kuitafuta amani, panakosekana mazungumzo, basi, ina maana ya uwepo wa mazingira ya kuvunjika kwa amani.

Na wanadamu sisi tumekuwa wepesi sana wa kunyosheana vidole na hata kuhukumiana pasipo kudadisi ili kuujua ukweli.

Na hapa nawaletea leo kisa cha wanandoa waliokaa miaka mingi bila kupata mtoto. Wakaamua wamfuge paka nyumbani. Naye paka huyo wakampenda sana kama mtoto wa kumzaa. Paka naye aliwapenda sana bwana na bibi nyumbani.

Ikatokea mke yule akapata mimba na hata kuzaa salama mtoto. Ikawa kama miujiza. Furaha nyumbani ikaongezeka.
Siku moja bwana na bibi walimwacha mtoto wao amelala kitandani.

Nao wakaenda zao kuwasabahi jamaa na marafiki.
Walipokaribia nyumba yao wakati wakirudi nyumbani wakshtuka sana. Walimwona paka wao nje ya mlango akiwa na kipande cha nyama mdomoni. Sura yake ilitapakaa damu pia.

Wote wawili wakachukua miche ya kutwangia nafaka. Kwa hasira wakamtwanga paka yule kichwani. Alikufa papo hapo.
Walipoingia chumbani wakamkuta mtoto wao amelala salama kitandani. Kando kuna nyoka mkubwa aina ya chatu.

Nyoka amekufa baada ya kujeruhiwa kwenye mapambano na paka.

Hell is the other people!- Jehanam ni wale wengine, lakini, pepo yaweza pia kuwa ni wale wengine.

Bob Lennon- Imagine...https://www.youtube.com/watch?v=VOgFZfRVaww

Ni Neno La Leo.

Maggid,

Image may contain: 4 people, people standing

 

Ni kwenye jumba la sinema pale Lumumba. Ni action film murua yenye maudhui mapya ya kiafrika zaidi ikiwamo mpangilio wa nyimbo. Mwanammke wa kiafrika anapewa nafasi kubwa pia. Ni mapinduzi. Nilifurahia pia kuiangalia filamu hii nikiwa na mke wangu mpenzi. 
Filamu imenikumbusha pia wimbo wa Gil Scott Heron...

Image may contain: 1 person, standing and outdoor


Ndugu zangu, 

Bado naamini Nchi Yetu ni ya amani na utulivu na yenye raia wapenda amani na watulivu.

Taarifa za kifo cha msichana huyu Mtanzania zimenisikitisha sana kama mzazi na Mtanzania. Fikra zangu nazielekeza kwa wazazi wa binti huyu. Hakuna jambo gumu kwa mwanadamu kama pale mzazi anapomzika aliyemzaa.

Rai yangu:

Nchi Yetu haijawa na tunavyokwenda sasa haitakuwa kama za wenzetu wenye kupandikiza chuki baina ya raia na hata kupelekea kuuana. 

Kama taifa, tufanye yote kuhakikisha Nchi Yetu inabaki kuwa ya amani na utulivu. 

Maana, tuna utamaduni tuliorithi wa kumaliza tofauti zetu kwa mazungumzo na katika mazingira ya kindugu. Tuna sifa kuu ambayo wengine hawana, nayo ni kuishi kwetu katika misingi ya Umoja wa Kitaifa bila kujali tofauti zetu za kidini, kikabila, itikadi wala rangi.

Tusikubali wachache watutumbukize kwenye yenye kupelekea roho za Watanzania wenzetu kupotea. Wenye kuhusika na masuala ya usalama waangalie taratibu zilizo bora na za kisasa za kuzuia kilichomtokea msichana huyu Aquiline kisitokee tena. Aidha, uchunguzi wa kina ufanyike kubaini chanzo na aliyehusika.

Mungu Ibariki Afrika,
Mungu Ibariki Tanzania.

Maggid.
 

 

Image may contain: 6 people, people smiling, people sitting

 

Ningependa kwenda tena Soweto nyakati hizi za utawala wa Ramaphosa.

Pichani ni Ijumaa moja, Novemba 2015, wenyeji wangu walinikaribisha Sakhumzi Restaurant and Bar , Soweto. Walinipa heshima kubwa kwa kujua natoka Tanzania. Maana nao wameniambia, kuwa utotoni wamesimuliwa habari nyingi na wazazi wao wapigania uhuru, juu ya taifa kubwa lenye uwezo wa kijeshi, kidiplomasia na watu wakarimu, Tanzania.

Maggid.

 

Saturday, 17 February 2018 07:45

Mcheza Mbali Na Kwao Hutuzwa Pia!


Ndugu zangu,

Kijana wetu John jana akiwa London aliwaongoza wenzake watatu kutetea kazi yao ya kisomi na kushinda. Wameshinda shindano lililoandaliwa na taasisi ya Lawyers Without Borders kwa kushika nafasi ya kwanza.
Shindano liliwashirikisha wasomi wa vyuo vikuu kadhaa vya UK. Kazi ya kisomi ya John na wenzake ilihusu Usafirishaji Haramu Wa Wanyama. ( Animal trafficking).
Kazi yao hiyo inatarajiwa kuchapwa kama kitabu cha kuelimisha jamii.
Hongera Sana John kwa kutuwakilisha Iringa!! pia!!
Maggid.

Image may contain: 3 people, people smiling, people sitting

 

Ndugu zangu,

Ili kuepuka hilo, dunia ya diplomasia imejiwekea taratibu zake za kidplomasia na kiungwana.

Hivyo, ukisikia Rais wa Jamhuri kamteua fulani kuwa Balozi kwenye nchi fulani, basi ujue, kuwa taratibu za awali za kidiplomasia zimeshafanyika na kukamilika.

Nilipata kufundishwa na rafiki yangu mwanadiplomasia, kuwa, jina la mteule hufikishwa kwanza kwenye mamlaka za nchi ambayo Rais wa Jamhuri angependa mtu huyo aende kumwakilisha.

Mamlaka za nchi ya kigeni hufanya upembuzi yakinifu. Maana yake ni kuwa itampekua mtu huyo kuhakikisha hana lolote ambalo kuwepo kwake kama balozi kwenye yao inaweza kuathiri maslahi ya nchi ya kigeni.

Na je, wakimkuta mteule ana mzoga kwenye kabati lake wenye athari kwa nchi yao?

Jibu, nchi ya kigeni haimkatai kwa sauti mteule wa Rais wa Jamhuri. Hukaa kimya muda mrefu bila kurudisha majibu ya kumthibitisha mteule.

Hapo ujumbe huwa umefika, taratibu za kupeleka jina jingine hufanyika.

Ni yepi ambayo hupelekea mteule akataliwe na nchi ya kigeni?

Jibu: Yaweza kuwa makubwa au madogo. Unayaoyaona madogo kama vile kutumia lugha zisizo na staha mtandaoni yanaweza kumnyima mtu nafasi ya ubalozi ugenini. Mfano, ni vigumu Wasaudia wakamthibitisha ubalozi mtu ambaye kupitia mitandao au maandiko ya vitabuni na magazetini ameukashifu mfumo wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia.

Hivyo hivyo, katika uhai wake, Christopher Mtikila asingeweza kuthibitishwa na India kuwa Balozi pale New Delhi wakati alikuwa na rekodi ya kutoa kauli za chuki kwa Wahindi ikiwamo kuwatukana kwa kuwaita Magabacholi!

Ndivyo ilivyo kwenye Diplomasia. Na kama nawe unaona vingine uje na hoja zako.

Maggid.

Image may contain: 1 person, text

 

Ndugu zangu,

Kuna wakati Mama Maria Nyerere alipata kuulizwa swali la kukera kutoka kwa mwandishi kijana.

Mwandishi huyo alimuuliza Mama Maria Nyerere:

“Hivi, inakuwaje Mwalimu ameondoka na kuacha familia yake ikiishi katika hali ya kawaida sana bila kuwa na mali nyingi wakati tunaona watendaji wa siku hizi wana mali na wengine wanasomesha watoto wao nje ya nchi?”

Mama Maria Nyerere alimjibu mwandishi yule:

“Naona wewe bado ni kijana sana, hukuwepo wakati ule wa Azimio la Arusha, lakini hiyo si sababu ya wewe kushindwa kufahamu ya nyuma, maana ulitakiwa kusoma.

Wakati wa Mwalimu kulikuwa na Azimio la Arusha na miiko ya viongozi. Na Mwalimu kama kiongozi, asingeweza kufanya tofauti na yale ambayo aliyasimamia na aliwataka wenzake katika uongozi wayafuate.”

Ndiyo, katika utaratibu wa hapo nyuma kidogo, na hasa baada ya kuondokana na kanuni, miiko na maadili ya uongozi ya enzi za Mwalimu, ilikuwa ni kawaida kukuta Watendaji wenye miradi ya biashara, mashamba na hata viwanda ambavyo wao wenyewe ndio wasimamiaji.

Hivi, Waheshimiwa hawa walipata wapi muda wa kusimamia biashara, mashamba na viwanda vyao kama si kuiba muda wa kuwatumikia wananchi na hata kutumia rasilimali za umma?

Inahusu swali hili; Ni nani atauzima mshumaa wa Serikali? Hapa kuna kisa nilichopata kusimulia.

Naam, miongoni mwa viongozi waliopata kuongoza dola ya Kiislam, hususan baada ya Mtume Muhammad (SAW) na baada ya masahaba, ni Amir muumini na Khalifa Umar bin Abdulaziz.

Wanazuoni wa Kiislamu wanatwambia, kwa utawala wa Khalifa Umar bin Abdulaziz ulijaa uadilifu. Si kwa viongozi tu, hata kwa raia wake.

Inasemwa kwamba moja ya mafanikio makubwa ya utawala wa Khalifa Umar bin Abdulaziz, ni kukusanya zakka. Katika Uislamu, zakka ni ibada ya lazima kwa mwenye nacho kuwapa masikini, yatima, wajane, wasafiri, raia na wengineo wenye kuhitaji.

Watu walijengewa imani kubwa, kiasi hakuna aliyethubutu kukwepa kutoa zakka. Hata wale waliopokea zakka walikuwa waadilifu, hawakupokea zakka mara mbili kama walishapokea kabla. Wote waliostahili kupata zakka , walipata zakka. Hakika, zakka zilitolewa zikajaa mabohari.

Siku moja raia mmoja alikwenda kwenye ofisi ya Khalifa Umar bin Abdulaziz. Wakati wa maongezi yao, Khalifa Umar alikuwa akihangaika kuupuliza na kuuzima mshumaa mmoja na kuwasha mwingine.

Alikuwa na mishumaa miwili mezani. Kadri mazungumzo yalivyoendelea, Umar aliendelea kufanya hivyo. Alipuliza mshumaa mmoja ukazimika, kisha akawasha mwingine.

Jambo hilo lilimstaajabisha sana mgeni wa Khalifa Umar bin Abdulaziz. Akauliza:

"Je; ni kwanini unazima mshumaa huu na kuwasha mwingine, kisha huo nao unauzima na kuwasha ule wa kwanza?

Khalifa Umar bin Abdulaziz akamjibu:

"Mshumaa huu ni wa Serikali, wewe unaponiuliza habari za Serikali, nauwasha. Lakini naona mara unauliza habari za familia yangu, ndiyo maana nauzima wa Serikali na kuuwasha mshumaa wangu mwingine nilioununua kwa pesa za mfukoni mwangu. Nachelea nisije fanya dhuluma kwa mali ya nchi."

Ndugu zangu, 
Bila shaka, hicho ni kisa chenye kutupa mafundisho muhimu
juu ya dhana nzima ya maadili katika utumishi wa umma. Tafakari!

Maggid,

Image may contain: 3 people, people smiling, people sitting


Ndugu zangu, 

Kupitia taarifa ya habari usiku huu nimezipokea taarifa kuwa Rais wa Jamhuri, Dr. John Magufuli amemtua Dr. Wilbroad Slaa kuwa Balozi wetu nchini Sweden.

Binafsi nimezipokea kwa furaha taarifa hizo. Rais wa Jamhuri ameonyesha umakini mkubwa kwenye teuzi zake ikiwamo hii ya Dr. Slaa kwenda Sweden.

Kimsingi Dr. Slaa ataiwakilisha nchi yetu Scandinavia yote ikiwamo nchi za Denmark, Finland na Norway hata Estland.

Binafsi nampongeza rafiki yangu na Mjamaa mwenzangu ( Social Democrat) Dr. Slaa kwa kupewa heshima hii kubwa kutuwakilisha kwenye nchi muhimu kwetu kihistoria na wakati huu kwenye mwelekeo wa diplomasia ya kiuchumi.

Karibu sana Sweden Dr Slaa! Valkommen Till Sverige!

PS: Pichani kamanda wangu huyo Manfred akiwa kwenye picha na Dr Slaa mwaka 2015 pale Mikumi. Mwaka huu yeye na pacha mwenzake Gustav wamehamia Sweden kimasomo, na sasa Dr. Slaa ndiye Balozi wao!Ameacha nyuma yake simulizi mbaya za ufisadi akitumia ofisi kuu ya Jamhuri. Inasikitisha.

Maggid.

Page 1 of 3154

Tafuta Habari

Blog Shabihana

Simu