habari

Siku Ya Afya Duniani, Ummy Mwalimu Aeleza Hatua Za Serikali Katika Kuboresha Huduma Za Afya.

on

Ndugu Wananchi

Siku ya Afya duniani huadhimishwa tarehe 7 Aprili ya kila mwaka. Kauli mbiu ya mwaka huu ni HUDUMA BORA ZA AFYA KWA WOTE.  Kauli mbiu  inatutaka kuhakikisha kuwa hukuna mtu anayekosa huduma za afya popote alipo. Napenda kuchukua fursa hii kuwafahamisha wananchi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe Rais Dr. John Pombe Magufuli inaendelea kuchukua hatua mahususi za kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa kila mtanzania mahali popote alipo bila kikwazo. Hatua tulizochukua ni pamoja na kuongeza rasilimali fedha kwa kugharamia huduma za afya, kuimarisha huduma za chanjo kwa watoto, kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto ikiwemo huduma za uzazi za dharura, kupanua huduma za matibabu ya kibingwa sambamba na kuimarisha mifumo ya kutoa huduma za afya.

Ndugu wananchi

Tangu tumepata Uhuru, Serikali imehakikisha inawapatia wananchi wake huduma bora za Afya bila kikwazo cha aina yoyote. Katika kuhakikisha dhana hii ya Upatikanaji wa huduma za afya kwa wote na kwa uhakika (Universal Health Coverage – UHC), Serikali imekuwa na mipango na mikakati mbalimbali ya kutekeleza azma hiyo.  Utekelezaji wa Mikakati hiyo unawiana na dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kwamba Matokeo ya Malengo Endelevu ya Dunia (SDGs) na mipango ya nchi katika kuelekea uchumi wa Viwanda na middle income Country yanafikiwa.

Ndugu Wananchi

Serikali imekuwa ikitoa kipaumbele kwa sekta ya Afya kwa kutenga fedha kwa ajili ya Kugharamia utoaji wa huduma za Afya Nchini. Kiwango cha Fedha kinachotengwa  katika Sekta ya Afya kimeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka, ambapo katika mwaka wa fedha 2016/17 Sekta ya afya ilitengewa kiasi cha shilingi trilioni 1.9 na mwaka 2017/18 ilifikia shilingi trilioni 2.2. Mwenendo huu unaonyesha kumekuwepo na juhudi kubwa ya Serikali katika kuipa Sekta ya afya kipaumbele ili iweze kutekeleza mipango ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi wote.

Ndugu Wananchi

Serikali imeendelea kuhakikisha hali ya upatikanaji wa dawa inaboreshwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini ili kuondoa kero kwa wananchi ya kukosa huduma ya dawa wanapokwenda kutibiwa katika vituo vya umma vya kutolea huduma za Afya. Katika mwaka 2017/18, Serikali imetenga Kiasi cha Shilingi bilioni 269 kwa ajili ya kununua na kusambaza dawa, vifaa, vifaa tiba, na vitendanishi ikilinganishwa na kiasi cha Shilingi bilioni 31 kilichotengwa mwaka 2015/2016. Hali hii imewezesha upatikanaji wa dawa muhimu 135 katika Bohari ya Dawa (MSD) kwa kiwango cha wastani wa asilimia 81 katika kipindi cha Februari 2018. Aidha hali ya upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya ilifikia kuwa asilimia 89.6 katika kipindi hicho.

Ndugu Wananchi

Wizara imeendelea kutoa huduma za Chanjo kulingana na Sera na Miongozo. Aidha, Wizara kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo, imehakikisha kuwepo kwa chanjo za kutosha kwa ajili ya huduma za chanjo kwa watoto na makundi mengine kwa kununua na kusambaza chanjo katika Mikoa na Halmashauri zote nchini.  Mwezi Desemba, 2017 nchi yetu ilipongezwa kwa kufanya vizuri katika utoaji wa huduma za chanjo nchi yetu imekua miongoni mwa nchi zilizofanya vizuri katika utoaji wa huduma za chanjo kwa mwaka 2016, ambapo tuliweza kuvuka lengo kwa kufikia kiwango cha chanjo cha asilimia 97 na kuwa nchi ya tatu kati ya nchi zinazofanya vizuri katika utoaji wa chanjo baada ya nchi ya Zambia (99%) na Rwanda (98%)

Ndugu Wananchi

Katika kupunguza vifo vya Wanawake wajawazito na watoto wachanga, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya nchini na kusogeza huduma za Afya kwa kujenga vituo vipya 268 na hivyo kufanya vituo vya kutolea huduma za Afya kufikia 7,284 kwa hivi sasa, ikilinganishwa na vituo 7,014 vilivyokuwepo mwaka 2014/2015.  Vilevile, tumechukua hatua za kuboresha vituo vya Afya  (Health Centres) 220 kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI ili kuviwezesha kutoa huduma za uzazi za dharura kwa kujenga na kukarabati majengo ya upasuaji (Theatre),  Wodi za Wazazi na Watoto, Maabara ya damu na nyumba za watumishi ili kusogeza karibu na wananchi huduma za uzazi za dharura ikiwemo upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni. Hadi Desemba 2015, ni Vituo vya Afya vya Serikali  (Health Centres) 117 tu (sawa na asilimia 21) kati ya vituo vya Afya vya 473 vinavyoweza kutoa huduma ya upasuaji wa dharura kwa wajawazito. Hakuna shaka kuwa jitihada hizi za Serikali ya Awamu ya Tano za kupanua huduma za upasuaji wa dharura ni sehemu ya kuwezesha Huduma bora za afya kwa wanawake wajawazito hasa wa vijijini.

Ndugu Wananchi,

Katika kuhakikisha huduma za matibabu ya kibingwa zinapatikana kwa wananchi wengi, serikali imeendelea na jitihada za kuboresha huduma za matibabu ya kibingwa zitolewazo nchini. Maboresho hayo, licha ya kuwa yanalenga katika kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopewa rufaa ya Matibabu nje ya nchi ili kupunguza gharama kubwa ambazo Serikali inaingia katika kupeleka wagonjwa nje ya nchi ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma za matibabu ya kibigwa kwa wananchi hasa wa kipato cha chini. Katika mwaka 2017/18 wanannchi waliopewa rufaa matibabu nje ya nchi ni 103 ikilinganishwa na watu 304 mwaka 2016/17. Mafanikio haya ni kutokana na maboresho yaliyofanyika katika Hospitali zetu za Kifaifa, ambapo kwa hivi sasa zimeongeza uwezo wa kutoa huduma za Kibingwa ambazo awali hazikuwa zikitolewa hapa nchini na hivyo kulazimu wagonjwa kupatiwa rufaa nje ya nchi. Huduma zilizoimarishwa ni pamoja na upandikizaji wa figo na vifaa vya kuongeza usikivu (Conchlea implants) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, upasuaji kwa kutumia tundu dogo na kufungua kifua katika Taasisi ya Jakaya Kikwete, Vilevile Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma za afya katika Taasisi ya Saratani Ocean Road ambapo dawa zinapatikana kwa asilimia 100 na muda wa kupata huduma ya mionzi ya Saratani imepungua kutoka muda wa miezi mitatu hadi wiki 6.

Ndugu Wananchi

Ili kufanikisha upatikanaji wa huduma za Afya kwa kila mwananchi, Serikali kupitia Wizara ya afya imeboresha mwongozo wa utoaji huduma katika ngazi ya Jamii. Mwongozo huu unatoa fursa ya kuwa na wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambao watafanya kazi chini ya usimamizi wa mkuu wa kituo cha afya yaani Zahanati, hadi sasa tuna wahitimu 8,857.

Ndugu Wananchi

Serikali ina mpango wa kuhakikisha kwamba wananchi wote wanajiunga katika mfumo wa Bima ya afya ili wawe na uhakika wa kupata huduma za afya pindi wanapozihitaji bila ya kikwazo cha fedha. Lengo ya Serikali ni kuhakikisha angalau asilimia 70 ya wananchi wote wanajiunga na kuchangia katika mfuko wa Bima ya Afya ifikapo mwaka 2020 kutoka asilimia 32 ya sasa. Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali imedhamiria kutunga Sheria itakayoanzisha Mfuko mmoja wa Bima ya Afya ambao kila mwananchi atapaswa kujiunga na kuchangia.

Hitimisho:

Katika kuadhimisha Siku ya Afya Duniani 2018, nitumie fursa hii kusisitiza tena kuwa ni dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kuhakikisha kuwa hakuna mwananchi atakayekosa huduma za bora za afya pindi anapozihitaji.

Asanteni.

Na Fullshangwe Blog.

About Hosea Revocatus

hosearevocatus9@gmail.com

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *