habari

SMZ kutumia dola milioni 10 kuwaendeleza wajasiriamali

on

 

Mohamed Khamis

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar  inatarajia kutumia dola za Marekani milioni 10  kwa ajili ya mkakati maalumu wa kuwasaidia wajasiriamali visiwani hapatia mikopo sambamba na mafunzo ambayo yatawawezesha kuberesha bidhaa zao.

Utekelezaji wa mkakati huo, ni wa miaka mitano na unatarajiwa kuanza Julai 2019 ambapo miradi 1,684 itawezeshwa kati ya hiyo miradi 495 ni mipya.

Hayo yalielezwa na katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda, Juma Ali Juma, alieleza hayo jana visiwani hapa na kusema kila kitu tayari kimekaa sawa.

Alisema katika programu hiyo, serikali itazingatia miradi ya wajasiriamali wanawake na vijana kwa asilimia 35, miradi ya viwanda na biashara asilimia 20, miradi ya wajasiriamali ya watu wenye mahitaji maalumu asilimia tano na miradi ya utalii asilimia 10 na asilimia zilizosalia zitatumika kwa miradi mengine ya pamoja.

Alisema programu hiyo itatolewa kwa mujibu wa  utaratibu kwa mjasiriamali mmoja mmoja hadi kikundi cha watu wanne.

Aidha alisema mkopo huo utaanzia shilingi 500,000 hadi milioni 10 ambazo zitapitishwa katika mfuko wa wajasiriamali.

Pia alisema, kutakuwa na kundi jengine la wajasiriamali watakaopata fursa ya mkopo huo ambao utatolewa na mfuko wa SMIDA kuanzia shilingi milioni 10 hadi milioni 57 ambapo kikundi hicho kitatakiwa kuwa na jumla ya watu 10 hadi 19.

Alisema kundi jengine litakalonufaika ni wajasiriamali wa kati ambao wana uwezo wa kuajiri ambapo fedha zao zitapitia Benki ya watu wa Zanzibar (PBZ).

Mbali na hilo, alisema miongoni mwa maeneo ambayo yatapewa kipaumbele ni pamoja na miradi ya kilimo, uvuvi, mifugo na mboga.

Katika hatua nyengine alisema, zoezi hilo litakuwa sambamba na miradi itakayoibuliwa na halmashauri na sekta husika ili kuhakikisha kunakuwa na ufanisi wa utekelezaji wenye kuleta tija.

Mapema alisema, mafanikio hayo yamekuja kufuatia ziara iliyofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein katika Nchi za Falme za Kiarabu   mwaka 2018 ambapo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliwasilisha hoja ya tatizo la ajira kwa vijana.

Alisema kufuatia mazungumzo hayo, Mfuko wa Khalifa Foundation kutoka nchini humo ulihamasika na hatimae kutuma ujumbe wake kufika nchini kwa ajili ya kuangalia miradi ya wajasiriamali.

Baadhi ya wajasiriamali visiwani hapa walisema pindi mkakati huo ukifanikiwa ni wazi kuwa watapiga hatua ikiwemo kujikwamua kiuchumi.

 

 

About Muhammed Khamis

hosearevocatus9@gmail.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *