simulizi

“Stori Ya Mkulima Mwamwindi Kumwua RC Kleruu Haikuandikika!”

on

Na Maggid Mjengwa.

Ndugu zangu, Kwenye utafiti wangu wa tukio la Desemba 25, 1971 nilikutana na kuongea na Mzee Hongole. Nilikutana nae Njombe mwaka 2011.

Mzee huyu pichani, alipata kuwa mwandishi wa habari kijana sana wakati tukio la Mwamwindi kumwua Mkuu wa Mkoa Dr Kleruu lililopotokea.

Nilimwuliza: Ulikuwa wapi wakati huo?

Jibu:

” Ndio kwanza nilikuwa nimepangiwa kufanya kazi kama mwandishi wa habari kwenye gazeti la kanisa pale Iringa.

Lilikuwa tukio kubwa sana. Kama mwandishi nilitamani sana kuandika habari za tukio lile. Nilianza kwa kukusanya maoni ya watu wa Iringa na kanda ya nyanda za juu.

Lakini, kwa wakati ule, mfumo haukuwa tayari kuona habari kama zile zinachapishwa.”

Aliniambia Mzee Hongole, ambaye, katika miezi ya mwisho ya uhai wake, alichagua kuliandikia gazeti la Kwanza Jamii. Mimi nilikuwa Mhariri wake mkuu. Mzee Hongole alifariki mwaka 2011.

Mzee Hongole alinieleza mengi aliyokusanya wakati ule. Kwamba raia waliogopa sana kusimulia. Lakini, chini chini walitoa maoni yao.

Kwamba mazingira ya wakati na baada ya tukio hayakuruhusu habari zile kuchapwa gazetini.

Kati ya niliyoyabaini katika kutafiti habari za mazingira yaliyopelekea tukio lile la Mkulima Mwamwindi na RC Kleruu, ni kuwa, ni wakati huu, waliokuwepo wakati huo, wamekuwa na hamu ya kukata kiu ya kusema waliyokuwa nayo moyoni.

Unaona pia, kuwa Mkulima Saidi Mwamwindi Na RC Kleruu kimsingi walikwazana katika jambo kuu ambalo, kama wangeelewana katika hilo, basi, Iringa ingelipata mwelekeo mwingine kabisa, na pengine ingeleta athari chanya kwa nchi.

Unaona pia, kuwa kuna watendaji chini ya Mwalimu Nyerere, ambao hawakumtafsiri vema mkuu wao, Rais wa Jamhuri. Hususan kwenye tafsiri ya sera na mipango ya nchi.

Maggid.
Iringa.

About Muhammed Khamis

hosearevocatus9@gmail.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *