habari

Taarifa Ya Jeshi La Polisi Mbeya.

on

KUPATIKANA NA POMBE HARAMU YA MOSHI @ GONGO.

Mnamo tarehe 02.08.2018 majira ya saa 16:30 jioni, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko eneo la Usongwe lililopo Kata ya Nsalala, Tarafa ya Usongwe, Wilaya ya Kipolisi Mbalizi, Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kumkamata HELENA ULEMBUSYA [30] Mkazi wa Nsalala akiwa na Pombe Haramu – Gongo ujazo wa lita 20. Mtuhumiwa ni muuzaji na mtumiaji wa pombe hiyo. Mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani mara upelelezi utakapokamilika.

KUPATIKANA NA NYARA ZA SERIKALI

Mnamo tarehe 02.08.2018 majira ya saa 15:50 jioni, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na askari wa TANAPA lilifanya msako huko katika Kijiji na Kata ya Madibira, Taràfa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali na kufanikiwa kumkamata FRANK KISINGA [30] Mkazi wa Nyamakuyu akiwa na ngozi ya simba na Mbao pori 3. Mtuhumiwa ni jangili na upelelezi zaidi unaendelea.

KUPATIKANA NA NOTI BANDIA.

Katika msako mwingine, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia SALOME PAUL [27] Mkazi wa Airport akiwa na noti 5 za bandia za Tshs 10,000/- zenye namba BF 1547978 noti – 4 na AA 4243052 noti 1.

Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 02.08.2018 majira ya saa 17:30 jioni katika msako uliofanyika huko Mtaa wa Ndogole, Kata Manga, Tarafa Sisimba, Jijini Mbeya. Upelelezi unaendelea ili kubaini mtandao mzima wa mtu/watu wanaojihusisha na uingizaji wa noti bandia katika mzunguko wa fedha.

KUPATIKANA NA SARE YA JESHI – JWTZ.

Mnamo tarehe 02.08.2018 majira ya saa 11:00 Asubuhi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko eneo la Mafiati, Kata ya Manga, Tarafa ya Sisimba, Jiji na Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kumkamata ANYEMKE ESSAU [31] Mkazi wa Iganzo akiwa na mkanda wa sare ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania – JWTZ. Upelelezi unaendelea.

Watuhumiwa watafikishwa Mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

TUKIO LA MAUAJI WILAYA YA MBEYA.

Mnamo tarehe 02.08.2018 majira ya saa 20:00 usiku huko eneo na Kata ya Mwakibete, Tarafa Iyunga, Jijini Mbeya, mtu mmoja ambaye amefahamika kwa jina la RAI SANGA [44] Mkazi wa Mwakibete alifariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi.

Inadaiwa kuwa marehemu alipigwa jiwe kubwa usoni na mtu/watu wasiofahamika akiwa njiani anarudi nyumbani kwake akitoka katika shughuli zake na alifariki dunia muda mfupi alipofikishwa Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa matibabu. Upelelezi unaendelea ili kuwabaini na kuwakamata waliohusika katika tukio hilo.

KUFANYA SHUGHULI ZA UGANGA BILA KIBALI @ LAMBALAMBA.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia JUMA RAMADHAN @ AKSON [24] Mganga wa kienyeji na mkazi wa Isikizya Mkoa wa Tabora kutokana na kufanya shughuli za uganga @ lambambala kwa kupiga ramli chonganishi.

Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 02.08.2018 majira ya saa 17:30 jioni huko Kijiji cha Lupaso kilichopo Kata ya Lwangwa, Tarafa ya Busokelo, Wilaya ya Rungwe.

Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kukabiliana na vitendo vya uhalifu na ajali za barabarani ili kuhakikisha kuwa wageni na wakazi wa Mkoa huu wanaendelea kuwa salama na mali zao. Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kushirikiana na wananchi na wadau wengine wa usalama hali inayopelekea kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu pamoja na ajali za barabarani.

WITO:

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ULRICH O. MATEI anatoa wito kwa jamii kuacha tama ya mali kwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu kwani uhalifu haulipi na badala yake wajishughulishe na kazi halali kwa ajili ya kujipatia kipato. Aidha Kamanda MATEI anatoa rai kwa wananchi kuachana na imani potofu za kishirikina kwani zinasababisha madhara makubwa kwa jamii.

About Muhammed Khamis

hosearevocatus9@gmail.com

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *