habari

Tangazo La Trump Kujiondoa Kwenye Mkataba Wa Kuzuia Silaha Za Nuklia Lapokelewa Kwa Hisia Tofauti.

on

Hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani, ya kutangaza kwamba nchi hiyo inajiondoa kwa mkataba wa kimataifa juu ya mpango wa kuizuia Iran kutengeneza silaha za nuklia, JCPOA, imearifiwa kupokelewa kwa hisia tofauti na wabunge wa Marekani na viongozi mbalimbali ulimwenguni kote.

Wabunge wengi wa chama cha Demokratik wameikosoa hatua hiyo huku Warepublikan wakiisifu.

Spika wa bunge, Paul Ryan, ambaye ni Mrepublikan, aliutaja mkataba huo kuwa uliokuwa na hitilafu kubwa.

Lakini kiongozi wa wachache kwenye bunge hilo, Nancy Pelosi alimshutumu Trump na kusema kwamba katika uamuzi wake, rais huyo hakutilia maanani ukweli kwamba mkataba huo ulikuwa unafanya kazi kama ulivyokusudiwa.Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, kupitia ujumbe wa Twitter amesema kuwa nchi yake, Ujerumani na Uingereza “zimesikitishwa mno na hatua hiyo ya Trump.”

Mapema Jumanne, Macron alisema kuwa Ufaransa itaendelea kuunga mkono mikakati ambayo itaimarisha usalama katika eneo hilo.

Katika hotuba iliyosubiriwa na wengi, RaisTrump alitangaza Jumanne kwamba ameamua kuiondoa Marekani kutoka mkataba wa kimataifa juu ya mpango wa kuizuia Iran kutengeneza silaha za nuklia, JCPOA.

Akizungumzia kutoka Ikulu, Trump alisema ataiwekea tena Iran vikwazo vikali vya kiuchumi vilivyondolewa wakati wa kufikiwa mkataba huo na mataifa mengine matano yenye nguvu duniani pamoja na Iran mwaka 2015.

Washirika wa Ulaya hasa Ufaransa, Uingereza na Ujerumani, wamekuwa wakijaribu kumshawishi kiongozi huyo kutochukua hatua hiyo ambayo wanasema ndio njia pekee ya kusimamia na kufuatilia harakati za nuklia za Iran.

Kabla ya hatua hiyo ya Trump, Iran ilikuwa imeeleza kwamba haingekubali kujadiliana tena juu ya mkataba mwengine na Marekani, na kwamba kwa kujiiondoa, Marekani ingekuwa inakiuka mkataba uliopo na kwamba itaendelea na mipango yake.

Wizara ya fedha ya Marekani ilitoa taarifa Jumanne kuwataka Wamarekani wote walioanza uhusiano na Iran chini na makubaliano hayo, kuanza kusitisha kazi zao.

About Hosea Revocatus

hosearevocatus9@gmail.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *