habari

TRA yawapa jukumu masheha ukusanyaji wa kodi Pemba

on

 

Na Mohamed Khamis

Katikaka kuhakikisha ukuaji wa mapato unaongezeka Nchini Masheha na Madiwani wilaya ya Mkoani Kisiwani Pemba, wametakiwa kushirikiana pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA)  ikiwemo kutoa taarifa za wale wote wanaokwepa kodi ikiwemo wafanya biashara.

Akizungumza katika mkutano wa kuelimisha masheha na madiwani kuhusu umuhimu wa kulipa Kodi, Afisa Mdhamini Idara ya Kodi za Ndani Hafidh Saleh Mohamed alisema, masheha na madiwani ni wadau wakubwa wa jamii, hivyo ni vyema wakachukua juhudi ya kuielimisha, ili wajue umuhimu wa kulipia kodi.

Alisema kuwa, ipo haja kwa masheha na madiwani kutoa taarifa za wafanyabiashara wanaokwepa kodi, kwani wao ndio wanaoikosesha Serikali mapato yake na kudumaza maendeleo ya nchi.

“Mapato ndio kila kitu, hivyo tushirikiane pamoja kuelimisha jamii na muwafichue wale ambao wanafanya biashara bila kulipa kodi, ili walipe na tupate mafanikio”, alisema.

Kwa upande wake Afisa Kodi kutoka TRA Unguja Omar Abdalla Kirobo alisema kuwa, bila ya kodi Serikali haiwezi kutekeleza majukumu yake ya kimaendeleo, kwani matumizi yake yote inategemea Kodi.

“Ni lazima watu wafahamu kwamba mapato yanayotokana na Kodi hutumika kugharamia huduma za kijamii, ili nchi iweze kukuwa kiuchumi na kupata maendeleo, wafanyabiashara wanatakiwa walipe Kodi”, alisema.

Nae Afisa Elimu na Huduma Abdalla Juma Abdalla kwa walipakodi TRA Zanzibar aliwataka masheha na madiwani kudhibiti biashara za magendo, ili kuongeza mapato ya nchi.

Afisa huyo alieleza kuwa, watumishi wa umma wana wajibu wa kulipia Kodi na kuhimiza wadau wao kufahamu na kutimiza wajibu wa kulipa kodi kwa hiari kwa mujibu wa Sheria.

“Pamoja na uwepo wa Sheria zilizoanzishwa bado kumekuwa na changamoto kadhaa katika usimamizi wa sheria kama maeneo ya biashara, ukusefu wa mifumo ama uwezo wa kugundua mapato na uhusiano, ukuaji wa watu ukilinganisha na mapato yanayokusanywa, kutotoa na kudai risiti”, alieleza.

Akifungua mkutano huo Afisa Ushirika kutoka Wilaya ya Mkoani Ali Mohamed Ali aliwataka masheha na madiwani hao kuielimisha jamii umuhimu wa kukusanya Kodi, ili wafanyabiashara wasidorore kukusanya mapato.

Sheha wa shehia ya Kengeja Mohamed Kassim alisema kuwa Kodi ndio muhimili mzima wa Serikali na kuwataka wenzake kuhakikisha wanasimamia na watekeleza yale waliyoelekezwa na bodi hiyo, ili kuipatia Serikali mapato yake.

Saumu Saleh Abdallan alisema kuwa, watashirikiana kuhakikisha wanaleta maendeleo katika nchi kwa kuihamasisha jamii kulipia Kodi kwa hiari.

Mkutano huo wa siku moja umeandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) umefanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkoani, lengo ni kuwaelimisha masheha na madiwani umuhimu wa kulipia kodi na wao kwenda kuielimisha jamii.

About Muhammed Khamis

hosearevocatus9@gmail.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *