habari

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Yatangaza Uchaguzi Mdogo Wa Udiwani Katika Kata 37

on

Mwandishi wetu
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 37 za Tanzania Bara zilizopo katika Halmashauri 27 na mikoa 13 ya Tanzania Bara,  utakaofanyika tarehe 13 Oktoba mwaka huu.
Akitangaza uchaguzi huo, Mwenyekiti wa NEC Jaji wa Mahakama ya Rufaa Semistocles Kaijage, alisema fomu za uteuzi wa wagombea katika uchaguzi huo zitatolewa kati ya tarehe 15 hadi 21 Septemba, mwaka huu.
Alisema uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 21 Septemba, mwaka huu wakati kampeni za Uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 22 Septemba hadi tarehe 12 Oktoba mwaka huu.
Jaji Kaijage alifafanua kuwa uchaguzi huo unafuatia Tume kupokea taarifa ya uwepo wa nafasi wazi za udiwani kwenye kata hizo kutoka kwa Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa kwa kutumia kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa.
“Baada ya kupokea taarifa hiyo na kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa; Tume ina utaarifu umma kuhusu kuwepo kwa Uchaguzi mdogo katika Kata hizo thelathini na saba (37).”, alisema Jaji Kaijage.
Kufuatia uchaguzi huo, Mwenyekiti huyo wa NEC alivialika Vyama vya Siasa, Wadau wote wa Uchaguzi na Wananchi kwa ujumla kushiriki katika Uchaguzi huo.
Aliongeza kwa kuviasa Vyama vya Siasa na Wadau wa Uchaguzi kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Madiwani), 2015, Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 na maelekezo yote yaliyotolewa au yatakayotolewa na Tume wakati wote wa Uchaguzi huo.
Wakati huo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewateua Madiwani watatu Wanawake wa Viti Maalum kujaza nafasi wazi za madiwani katika Halmashauri tatu za Tanzania Bara.
Akitangaza uteuzi huo, Mwenyekiti wa NEC Jaji wa Mahakama ya Rufaa Semistocles Kaijage, aliwataja madiwani hao kuwa ni Halima Salum Kisenga (CCM) wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigamboni.
Wengine walioteuliwa ni Emmy Anania Shemweta kupitia CCM katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto na Nuru Mwalimu Chuma kupitia Chama cha Wananchi (CUF) katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.
Jaji Kaijage alisema uteuzi huo umefanyika baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa, ambaye aliitarifu Tume kuwepo kwa nafasi wazi kupitia vyama hivyo baada ya walioteuliwa kufariki dunia na kujiuzulu.

About Muhammed Khamis

hosearevocatus9@gmail.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *