habari

Wajumbe wa Baraza la wawakilishi wajitokeza kuchangia damu

on

Harakati za uchangiaji damu salama visiwani Zanzibar zimeimarika na kuwa maradufu zaidi hususani katikja kipindi hichi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ambapo Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid, ameitaka jamii kuendelea kuchangia damu kwa hiari kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa hasa mama wajawazito, watoto na wanaopata ajali.

Alieleza hayo wakati akifungua zoezi la kuchangia damu kwa hiari  lililoandaliwa na baraza hilo kwa ajili ya kukidhi  mahitaji ya damu katika kipindi cha mwezi mtukufu wa ramadhani.

Alisema baraza hilo, limejumuika na watendaji wake na jamii iliyoizunguka katika zoezi hilo ili kupunguza changamoto inayowakabili wagonjwa katika hospitali ya vituo vya afya.

Aidha alisema, uzoefu unaonesha katika kipindi cha mwezi wa ramadhani mahitaji ya damu yanakuwa makubwa huku kasi ya uchangiaji ikipungua.

Alisema, jukumu la kuchangia damu linamgusa kila mtu hasa ikizingatiwa  maradhi  na ajali hayachagui  mtu wala hayana miadi,  hivyo  aliiomba jamii kuendeleza utamaduni huo.

Alitaja miongoni mwa faida anazozipata mchangiaji damu kuwa ni pamoja na kupunguza hatari ya  kupata maradhi ya moyo na kupungua madini chuma ambayo yakiwa mengi  hudhoofisha kazi za kuta za moyo.

Aliwaomba wanasiasa na viongozi wa dini kuihamasisha jamii juu ya umuhimu wa kuchangia damu.

Alisema katika zoezi hilo, baraza hilo litachangia  chupa 100 na kwamba  zoezi hilo litakuwa endelevu katika kila kipindi cha ramadhani.

Meneja Uhusiano wa Benki ya Damu, Bakari Hamad Magarawa, alisema, uamuzi wa chombo hicho kujitolea kuchangia damu kwa hiari ni wa kupigiwa mfano na unafaa kuigwa na wengine.

Alisema mahitaji ya damu  katika kipindi cha mwezi wa ramadhani   ni wastani wa  chupa 1,750  hadi sasa tayari zimekusanywa chupa  1,400 kati ya hizo 400 zimekusanywa Pemba.

Alisema ifikapo Mei 4 kutakuwa na bonaza la kitaifa la uchangiaji damu litakalofanyika Maisara ili kuhakikisha malengo waliojiwekea yanafikiwa ambalo litasimamiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi.

Mwakilishi wa viti maalumu,  Mwantatu Mbarak Khamis,  mara baada ya kuchangia damu katika zoezi hilo, alisema iwapo jamii itakuwa na mwamko wa kujitolea kuchangia damu, tatizo la damu litaondoka.

Mwakilishi wa jimbo la Malindi, Mohamed  Ahmada Salum, alisema utamaduni huo utatoa fursa na ushiriki mzuri wa wawakilishi katika jamii.

 

 

Imehaririwa na Muhammed Khamis

 

About Muhammed Khamis

hosearevocatus9@gmail.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *