habari

Wawekezaji Wazawa Wapewa Rai Kujenga Viwanda vya Dawa

on

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametoa rai kwa
wawekezaji wazawa na wafanyabiashara nchini kujenga viwanda vya dawa na vifaa vya
tiba hapa nchini ili kuongeza kasi ya ujenzi wa uchumi wa viwanda na kukuza ajira.
Rais Magufuli ametoa rai hiyo leo Jijini Dar es Salaam, kwenye hafla ya uzinduzi wa
magari 181 yenye thamani ya shilingi bilioni 20.7 ya kusambaza dawa na vifaa vya tiba
yaliyotolewa msaada na Shirika la Global Fund kwa Serikali ya Tanzania kupitia Bohari
ya Dawa (MSD).
“Asilimia 94 ya dawa zinanunuliwa nje ya nchi, hivyo wawekezaji wazawa watumie
changamoto hii kama fursa ya kuanzisha viwanda vya dawa na vifaa tiba hapa hapa
nchini kwetu,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alibainisha kuwa ujenzi wa viwanda hapa nchini utasaidia kuongeza ajira
kwa Watanzania hasa vijana pamoja na kupunguza gharama za kuagiza bidhaa nje ya
nchi zikiwemo dawa na vifaa vya tiba.
Aidha Rais Magufuli ametoa wito kwa wataalamu na wasomi wazawa wa masuala ya
afya na tiba kujiunga pamoja na kuanzisha viwanda vya dawa ili kuchochea uchumi wa
viwanda na kuongeza mapato.
“Tunapoteza shilingi bilioni 500 kila mwaka kwa ajili ya kununua dawa nje ya nchi lakini
tungekuwa na viwanda vyetu fedha hizo tungetumia kwenye mambo mengine ya
maendeleo,” alisisitiza Rais Magufuli.
Pia Rais Magufuli alisisitiza kuwa madereva watakaoajiriwa kuendesha magari hayo
mapya wachaguliwe kwa umakini ili kupata watu waaminifu watakaoweza kuyatunza
kwa manufaa ya Watanzania.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa Tanzania (MSD) Bw. Laurian
Bwanakunu ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli kwa
kuongeza bajeti ya ununuzi wa dawa kutoka bilioni 31 mwaka 2015/2016 hadi kufikia
bilioni 269 mwaka 2017/2018.
Pia Bwanakunu amewashukuru Global Fund kwa msaada huo wa magari ambayo
yataongeza kasi ya usambazaji wa dawa nchi nzima kila baada ya miezi miwili.
Bohari ya Dawa Tanzania (MSD) ilianzishwa mwaka 1994 kwa ajili ya kununua,
kuhifadhi na kusambaza dawa na vifaa vya tiba nchini kote.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kuwasili katika Ofisi za Bohari Kuu ya
Madawa wakati wa hafla ya kukabidhi magari 181 yatakayokuwa yakisafirisha
vifaa tiba na vitendanishi katika Mikoa na Halmashauri mbalimbali nchini. Hafla
hiyo ilifanyika jana Jumatatu Machi 26, 2018 katika Ofisi za MSD Keko Mwanga
Jijini Dar es Salaam.

Maafisa Waafisa wa Serikali wakijadiliana mambo mbalimbali wakati wa
kukabidhi magari 181 kwa Bohari Kuu ya Madawa (MSD) yatakayokuwa
yakisafirisha vifaa tiba na vitendanishi katika Mikoa na Halmashauri mbalimbali
nchini. Hafla hiyo ilifanyika jana Machi 26, 2018 katika Ofisi za MSD
Keko Mwanga Jijini Dar es Salaam.

Kiongozi wa Brass Band ya Jeshi la Polisi akiongoza uimbaji wa nyimbo
mbalimbali zilizokuwa zikitumbuiza wananchi waliofika kushudia makabidhiano
ya magari 181 kwa Bohari Kuu yaMadawa (MSD) yatakayokuwa yakisafirisha
vifaa tiba na vitendanishi katika Mikoa na Halmashauri mbalimbali nchini.

About Muhammed Khamis

hosearevocatus9@gmail.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *