siasa

Waziri Asimamishwa Kazi Kwa Kumchapa Kibao Mbunge Mwenzake.

on

Serikali ya Zambia kupitia Bunge la Nchi hiyo imemsimamisha kazi Waziri wa Jimbo la Lusaka Bowman Lusambo kwa kipindi cha muda wa mwezi mmoja baada ya kumpiga kibao mbunge Chishimba Kambwili wakiwa bungeni.

Spika wa Bunge hilo Patrick Matibini amesema ni jambo la kawaida wabunge kutumia lugha isiyofaa na kuleta mizozo lakini kwa kitendo hicho cha Waziri kumpiga kibao mbunge, si cha kuvumilika.

Ameongeza kuwa kitendo hicho kilifanyika mwezi Oktoba mwaka jana, na kwamba yeye kama spika ana wajibu wa kuhakikisha kwamba heshima na haiba ya Bunge inalindwa na inahifadhiwa wakati wote.

Kutokana na adhabu hiyo, Waziri Lusambo atasitishiwa baadhi ya huduma zinazotolewa bungeni kama marupurupu na mshahara kwa muda wa kipindi chote atachokuwa anatumikia adhabu hiyo.

 Imeelezwa kuwa mbunge huyo aliyepigwa kibao amekuwa akiwatukana maofisa wa Serikali kwa tuhuma za rushwa tangu atolewe kuwa Waziri wa Mawasiliano mwaka 2016, japo Serikali imekuwa ikikanusha tuhuma hizo.

Hata hivyo imeelezwa kuwa Waziri huyo alichukua sheria hiyo mkononi ya kumchapa kibao mara mbili baada ya kuona mbunge huyo anazungumza uongo juu ya Serikali.

About Muhammed Khamis

hosearevocatus9@gmail.com