habari

Waziri Kigwangalla Aagiza Ujenzi Wa Viwanda Vidogo Vya Asali Kwa Wilaya Zote Za Mikoa Ya Tabora Na Katavi

on

Na Hamza Temba – Tabora
*Ahamasisha kilimo cha Korosho kama zao mbadala la kuinua uchumi na uhifadhi wa mazingira
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla ameuagiza Mfuko wa Ruzuku wa Misitu Tanzania (TAFF) kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuanzisha mradi wa viwanda vidogo vya kusindika na kufungasha asali katika mikoa ya Tabora na Katavi ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kujenga uchumi wa viwanda.
Ametoa agizo hilo jana kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mtakuja wilaya ya Skonge mkoani humo ikiwa ni muendelezo wa ziara zake mikoani kwa ajili ya kukagua shughuli za uhifadhi na kutatua changamoto zake.
Alisema kwa kiwango kikubwa wananchi wa mikoa hiyo wamekuwa wategemezi kwenye zao moja tu la tumbaku ambalo sio rafiki kwa mazingira kwakuwa miti mingi hukatwa kwa ajili ya kukausha zao hilo jambo ambalo ni muhimu sasa kuwekeza zaidi kwenye mazao mengine ikiwemo viwanda vya kusindika na kufungasha asali ili kuongeza uzalishaji, ubora na hatimaye kuongeza kipato na faida zaidi.
“Mwaka huu ule mfuko wa misitu, kwa kiasi kikubwa tuamue tuwekeze ukanda huu wa magharibi  ambapo kuna zaidi ya asilimia 60 ya misitu yote hapa nchini, na tuanze kwa kujenga kiwanda kimoja katika kila wilaya, ikiwemo Nzega, Skonge, Uyui, Tanganyika, Mlele, Mpanda na Kaliua.
“Tuwawezeshe wananchi wajiunge katika vikundi, tuwagawie mizinga ya kisasa, wafuge nyuki kisasa, warine asali kisasa, wakisharina wapeleke kwenye viwanda, ifungashwe kisasa, ipate bei kubwa, na mwisho wa siku wataona faida ya kuwa na misitu.
“Hapo tutakuwa tumewasaidia, watapa kipato mbadala lakini watakua wakali sana kwa watu wanaoharibu misitu na tutatengeneza jeshi kubwa la wananchi la ulinzi wa misitu yetu, hivyo nataka mradi huu uanze mara moja bila kusuasua ili na sisi tuchangie jitihada za Serikali ya awamu ya tano katika ujenzi wa uchumi wa viwanda. ” alisema Dk. Kigwangalla.
Wakati huo huo, Waziri Kigwangalla amewashauri wananchi wa mikoa hiyo kuanzisha kilimo cha korosho kama zao jingine mbadala la kuongeza kipato na kunusuru misitu badala ya kujikita kwenye zao moja la tumbaku ambalo ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa misitu ya mikoa hiyo.
Amesema ni muhimu walau kwa kila kaya moja kuanza kwa kupanda ekari moja ya mikorosho ili kuongeza zao jingine mbadala la biashara ambalo lina tija zaidi kiuchumi na kiuhifadhi wa mazingira.
“Kilimo cha tumbaku sio rafiki kwa mazingira tumejaribu kuleta mabani banifu yanayotumia kuni chache,  tumejaribu kuwashawishi wananchi wapande miti lakini tumechemsha, miti mingi imeendelea kukatwa misitu nayo inateketea siku hadi siku, ni lazima tutafute mbinu mbadala ya kukabiliana na changamoto hii, na hii ni kupitia zao hili la korosho” alisema Dk. Kigwangalla.
Amesema tafiti zinaonyesha kuwa zao la korosho katika mikoa hiyo lina uwezo wa kustawi zaidi na kuzalisha mara mbili kuliko mikoa ya kusini ambayo inasifika zaidi kwa uzalishaji huo hapa nchini.
Aidha ameziagiza halmashauri zote za mikoa hiyo kufanya utaratibu wa kupata mbegu na miche ya zao hilo mapema iwezekanavyo kwa ajili ya kuwagawia wananchi kabla ya msimu wa mvua kuanza na wataalamu wa kilimo wawaelimishe wananchi njia bora ya kupanda na kutunza miche hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Skonge, Peres Magiri alisema kiwango cha mvua kwa mwaka katika wilaya hiyo kimeshuka na kufikia 600mm kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na uharibifu wa mazingira.

About Muhammed Khamis

hosearevocatus9@gmail.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *