habari

Waziri wa elimu Z’bar ataka mashirikiano na zaidi na wadau

on

 

Muhamed khamis

Unguja.Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Riziki Pembe Juma ameitaka jamii kushirikiana na mamlaka zinazoshughulikia masuala ya udhalilishaji ili kuondosha muhali na kutokomeza vitendo hivyo hasa kwa wanawake na watoto.

Akifungua warsha ya siku sita ya kuwajengea uwezo Wakuza Mitaala wa Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu Zanzibar, katika ukumbi wa Mtakwimu Mkuu wa Serikali Mazizini Unguja amesema ni vyema kuondoa muhali na kuacha kuwapa hifadhi wahalifu wa vitendo hivyo kwani kutasaidia watoto kuishi katika mazingira salama.

Amesema kuna baadhi ya walimu na wanafunzi wa vyuo vikuu hapa nchini hawajielewi na hawajitambui, na hivyo kufanya vitendo ambavyo haviendani na maadili ya nchi, hivyo amewataka washiriki hao kutoka na maazimio sahihi ya kupinga vitendo vya udhalilishaji hasa katika sekta ya elimu ili Taifa liwe na watoto imara watakaoiongoza nchi yao.

Riziki amefahamisha kuwa masuala ya mitaala ndio miongozo yenye mpangilio wa mambo kwa wanafunzi ambao wanatakiwa kusaidiwa na kujua hatua kwa hatua katika kupata taaluma.

Hivyo amewataka Wakuza mitaala hao kujua vyema Sera ya Elimu, na msimamo wa Wizara hiyo juu ya maudhui ya namna ya kuyaingiza masuala hayo ya udhalilishaji katika mitaala yao.

Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt Idrisa Muslim Hija amewataka washiriki wa warsha hiyo ya Wakuza Mitaala kujadili kwa kina juu vitendo vya udhalilishaji hasa kwa watu wenye mahitaji maalum ili kuwasaidia katika kuondokana na janga hilo.

Wakiwasilisha mada juu ya hali ya maambukizi ya Ukimwi kwa vijana wa Zanzibar Mkuu wa sera na mipango kutoka Tume ya ukimwi Zanzibar ZAC Bi Halima Ali Mohamed amesema wasichana wengi hivi sasa wako katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU kutokana na kufanya mapenzi kinyume na maumbile kwa kuhofia kupata ujauzito au kupoteza usichana wao.

Hata hivyo amesema kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshuhulikia Watoto Duniani UNICEF ni asilimia 39.7 tu ya vijana wa Zanzibar ndio wanaofanya ngono ndani ya ndoa na waliobakia wanafanya ngono kabla ya ndoa hali ambayo ni hatari kwa maisha yao.

Warsha hiyo ya Siku sita imeandaliwa na Kitengo cha Elimu Mjumuisho na Stadi za Maisha cha Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kwa Kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu UNESCO.

About Muhammed Khamis

hosearevocatus9@gmail.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *